4 Mtaletewa maji kidogo ili mnawe miguu na kupumzika chini ya mti.
5 Wakati mnapopumzika, nitaandaa chakula kidogo, mle, ili mpate nguvu za kuendelea na safari yenu; maana mmenijia mimi mtumishi wenu.” Nao wakasema, “Sawa! Fanya kama ulivyosema.”
6 Abrahamu akarudi haraka hemani akamwambia Sara, “Tayarisha haraka vipimo vitatu vya unga bora, uukande, uoke mikate.”
7 Kisha akatoka haraka akaenda kwenye kundi la ng'ombe, akachagua ndama mmoja mzuri na mnono, akamkabidhi mtumishi ambaye aliharakisha kumchinja na kumpika.
8 Halafu Abrahamu akachukua siagi, maziwa na ile nyama iliyotayarishwa, akawaandalia wageni hao chakula; naye akasimama karibu nao kuwahudumia walipokuwa wakila chini ya mti.
9 Wale wageni wakamwuliza, “Mkeo Sara yuko wapi?” Abrahamu akawajibu, “Yumo hemani.”
10 Mmoja wao akasema, “Hakika nitakurudia wakati kama huu mwakani, na mkeo Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Sara alikuwa huko nyuma mlangoni mwa hema, akisikiliza.