7 Kisha akatoka haraka akaenda kwenye kundi la ng'ombe, akachagua ndama mmoja mzuri na mnono, akamkabidhi mtumishi ambaye aliharakisha kumchinja na kumpika.
8 Halafu Abrahamu akachukua siagi, maziwa na ile nyama iliyotayarishwa, akawaandalia wageni hao chakula; naye akasimama karibu nao kuwahudumia walipokuwa wakila chini ya mti.
9 Wale wageni wakamwuliza, “Mkeo Sara yuko wapi?” Abrahamu akawajibu, “Yumo hemani.”
10 Mmoja wao akasema, “Hakika nitakurudia wakati kama huu mwakani, na mkeo Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Sara alikuwa huko nyuma mlangoni mwa hema, akisikiliza.
11 Abrahamu na Sara walikuwa wakongwe, naye Sara mambo ya kawaida ya wanawake yalikuwa yamekoma kitambo.
12 Kwa hiyo, Sara alicheka kimoyomoyo akisema, “Mimi ni mzee, na mume wangu hali kadhalika. Je, nikiwa mzee hivi, nitaweza kufurahi na kupata watoto?”
13 Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kujiuliza kama kweli itawezekana apate mtoto akiwa mzee?