18 Wazawa wa Ishmaeli walikaa katika eneo lililo kati ya Hawila na Shuri, mashariki ya Misri, kuelekea Ashuru. Walikaa kwa utengano na wazawa wengine wa Abrahamu.
19 Hawa ndio wazawa wa Isaka mwana wa Abrahamu.
20 Isaka alipokuwa na umri wa miaka arubaini alimwoa Rebeka, binti Bethueli, Mwaramu wa Padan-aramu. Rebeka alikuwa dada yake Labani.
21 Rebeka alikuwa tasa, kwa hiyo Isaka akamwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akakubali ombi lake, Rebeka akapata mimba.
22 Mimba hiyo ilikuwa ya mapacha. Watoto hao wakashindana tumboni mwake Rebeka, naye akasema, “Kama hivi ndivyo mambo yalivyo, ya nini kuishi?” Basi, akaenda kumwuliza Mwenyezi-Mungu.
23 Mwenyezi-Mungu akamwambia,“Mataifa mawili yamo tumboni mwako;makabila mawili yatakayozaliwa nawe, yatafarakana.Moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine;mkubwa atamtumikia mdogo.”
24 Siku zake za kujifungua zilipotimia, Rebeka alijifungua mapacha.