18 Kisha ndugu zake wakamjia, wakainama mpaka chini mbele yake, wakasema, “Tazama, sisi tu watumishi wako.”
19 Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope, je, mimi ni badala ya Mungu?
20 Nyinyi mlitaka kunitendea vibaya, lakini Mungu alikusudia mema ili watu wengi wapate kuwa hai kama mwonavyo leo.
21 Haya, msiogope. Mimi nitawapeni chakula pamoja na watoto wenu.” Basi akawafariji na kusema nao vizuri.
22 Yosefu akaendelea kukaa katika nchi ya Misri pamoja na jamaa yote ya baba yake. Aliishi kwa muda wa miaka 110.
23 Yosefu alijaliwa kuwaona watoto na wajukuu wa mwanawe Efraimu, na pia kuwapokea kama wanawe watoto wa Makiri mwana wa Manase.
24 Baadaye Yosefu aliwaambia ndugu zake, “Mimi sasa ninakaribia kufa. Lakini Mungu hakika atawajia kuwasaidia. Atawatoa katika nchi hii na kuwapelekeni katika nchi aliyowaapia Abrahamu, Isaka na Yakobo.”