17 Hakika, Farao pamoja na jeshi lake kubwa hataweza kumsaidia vitani wakati Wababuloni watakapomzungushia ngome na kuta ili kuwaua watu wengi.
18 Kwa kuwa alikidharau kile kiapo na kuvunja lile agano ambalo aliahidi kwa mkono wake mwenyewe na kufanya mambo haya yote, hakika hataokoka.
19 “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema, kama niishivyo, kwa vile amekidharau kiapo alichoapa kwa jina langu na agano langu akalivunja, hakika nitamwadhibu vikali.
20 Nitatandaza wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu; nitampeleka mpaka Babuloni na kumhukumu kwa sababu ya uhaini alioufanya dhidi yangu.
21 Majeshi yake hodari yatauawa kwa upanga na watakaosalia hai watatawanyika pande zote. Hapo mtatambua kuwa mimi, naam, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
22 Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi mwenyewe nitachukua kisehemu cha ncha ya juu ya mwerezi, naam, nitavunja tawi changa kutoka matawi yake ya juu na kulipanda juu ya mlima mrefu sana.
23 Naam, nitalipanda juu ya mlima mrefu wa Israeli ili lichanue na kuzaa matunda. Litakuwa mwerezi mzuri, na ndege wa aina zote watakaa chini yake pia watajenga viota vyao katika matawi yake.