21 Majeshi yake hodari yatauawa kwa upanga na watakaosalia hai watatawanyika pande zote. Hapo mtatambua kuwa mimi, naam, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
22 Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi mwenyewe nitachukua kisehemu cha ncha ya juu ya mwerezi, naam, nitavunja tawi changa kutoka matawi yake ya juu na kulipanda juu ya mlima mrefu sana.
23 Naam, nitalipanda juu ya mlima mrefu wa Israeli ili lichanue na kuzaa matunda. Litakuwa mwerezi mzuri, na ndege wa aina zote watakaa chini yake pia watajenga viota vyao katika matawi yake.
24 Ndipo miti yote nchini itajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu huiporomosha miti mirefu na kuikuza miti mifupi. Mimi hukausha miti mibichi na kustawisha miti mikavu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema hayo na nitayafanya.”