14 Nitakufanya kuwa jabali tupu; utakuwa mahali pa wavuvi kukaushia nyavu zao, wala hutajengwa tena. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
15 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia hivi wewe Tiro: Wakazi wa sehemu za pwani watatetemeka watakaposikia kishindo cha kuanguka kwako na mlio wa majeruhi na wa watu wanaouawa.
16 Wakuu wote wa mataifa ya pwani watashuka toka viti vyao vya enzi, na kuvua mavazi yao ya heshima pamoja na nguo zao zilizotariziwa. Wakiwa wamejaa hofu, wataketi chini; nao watatetemeka wakati wote na kushangaa mno juu ya hayo yaliyokupata.
17 Wataimba utenzi huu wa kuomboleza:Umeangamizwa wewe mji maarufu,umetoweka kutoka baharini!Wakazi wake walieneza nguvu zao juu ya bahari,ambapo walihofiwa na wote.
18 Sasa watu wa bara wanatetemekakwa sababu ya kuanguka kwake;wakazi wa pwani, wametishika kwa kutoweka kwako!
19 “Maana, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakufanya wewe Tiro kuwa mahame, kama miji isiyo na watu, nitakapoleta juu yako maji kutoka vilindi vya bahari, na maji mengi yatakufunika.
20 Nitakuteremsha shimoni ili ujiunge na walioko huko, walioishi duniani zamani; nitakufanya ukae huko katika mahame milele. Hutakaliwa na watu milele na hutakuwa na nafasi miongoni mwa nchi za walio hai.