14 Bidhaa zako uliziuza huko Beth-togarma ili kujipatia farasi wa mizigo na wa vita, ngamia na nyumbu.
15 Watu wa Dedani walifanya biashara nawe. Nchi nyingi za pwani zilikuwa masoko yako maalumu. Watu wake walikuletea pembe za ndovu na mipingo kulipia bidhaa zako.
16 Watu wa Edomu walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako. Kwa kupata bidhaa zako walikupa akiki, vitambaa vya urujuani, vitambaa vilivyonakshiwa, kitani safi, matumbawe na yakuti.
17 Hata watu wa Yuda na Israeli walifanya biashara nawe; walikupa ngano, zeituni, tini za mwanzoni, asali, mafuta na marhamu kulipia bidhaa zako.
18 Watu wa Damasko walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako; walikupa divai kutoka Helboni na sufu nyeupe.
19 Vedani na Yavani walisafirisha bidhaa zako toka Uzali; hata chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai ili kupata bidhaa zako.
20 Watu wa Dedani walifanya biashara nawe kwa kukupatia matandiko ya farasi.