22 “Waashuru wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Wote waliuawa vitani,
23 na makaburi yao yako sehemu za chini kabisa shimoni kwa wafu. Wanajeshi wao wote waliuawa vitani na makaburi yao yamewazunguka. Hapo awali, walipokuwa wanaishi bado, walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.
24 “Waelamu pia wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao waliouawa vitani. Wote hao wasiomjua Mungu walishuka kwenye nchi ya wafu. Walipokuwa wanaishi bado walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Lakini sasa wanabeba aibu yao pamoja na wanaoshuka shimoni kwa wafu.
25 Wamelazwa na jeshi lao miongoni mwa wale waliouawa vitani. Wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wake wote waliouawa vitani na ambao wote hawamjui Mungu. Walipokuwa bado wanaishi walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai, na sasa wako hapo wamejaa aibu pamoja na wale waliouawa vitani.
26 “Watu wa Mesheki na wa Tabali wote wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Watu hao wote wasiomjua Mungu walikufa vitani, watu ambao walipokuwa hai walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.
27 Hao wasiomjua Mungu hawakuzikwa pamoja na mashujaa wa kale, ambao walikwenda kuzimu kwa wafu wakiwa na silaha zao, mapanga yao chini ya vichwa vyao na ngao zao juu ya miili yao. Mashujaa hao walipokuwa wanaishi bado walijaza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.
28 Basi, nyinyi Wamisri mtaangamizwa na kulazwa miongoni mwa wasiomjua Mungu waliouawa vitani.