3 Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi lao, akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Waisraeli wakawaangamiza kabisa Wakanaani pamoja na miji yao. Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Horma.
4 Waisraeli walifunga safari kutoka Mlima Hori wakapitia njia inayoelekea bahari ya Shamu ili waizunguke nchi ya Edomu. Lakini njiani watu walikufa moyo.
5 Basi, wakaanza kumnungunikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini mmetutoa Misri tuje tukafie humu jangwani? Humu hamna chakula wala maji; nasi tumechoshwa na chakula hiki duni.”
6 Hapo Mwenyezi-Mungu akapeleka nyoka wenye sumu miongoni mwa watu, wakawauma hata Waisraeli wengi wakafa.
7 Basi, watu wakamwendea Mose, wakamwambia, “Tumetenda dhambi kwa kumnungunikia Mwenyezi-Mungu na wewe pia. Mwombe Mwenyezi-Mungu atuondolee nyoka hawa.” Kwa hiyo, Mose akawaombea watu.
8 Ndipo Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona.”
9 Basi, Mose akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama nyoka huyo wa shaba, alipona.