27 Punda alipomwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, akalala chini. Balaamu akawaka hasira, akampiga kwa fimbo yake.
28 Hapo Mwenyezi-Mungu akakifunua kinywa cha huyo punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini hata ukanipiga mara hizi tatu?”
29 Balaamu akamwambia punda, “Wewe umenidhihaki! Kama ningekuwa na upanga ningalikuulia mbali sasa hivi!”
30 Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si yuleyule punda wako aliyekubeba maisha yako yote hadi siku hii ya leo? Je, nimewahi kukutendea namna hii?” Balaamu akajibu, “La.”
31 Hapo, Mwenyezi-Mungu akayafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Balaamu akajitupa chini kifudifudi.
32 Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Mbona umempiga punda wako mara hizi tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya.
33 Punda wako ameniona akaniepa mara hizi tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha hai punda huyu.”