1 Vifuatavyo ni vituo ambavyo Waisraeli walipiga kambi walipotoka Misri wakiwa katika makundi ya makabila yao chini ya uongozi wa Mose na Aroni.
2 Mose aliandika jina la kila mahali walipopiga kambi, kituo baada ya kituo, kwa agizo la Mwenyezi-Mungu.
3 Waisraeli waliondoka mjini Ramesesi mnamo siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, siku moja baada ya Pasaka ya kwanza. Waliondoka kwa uhodari mkubwa mbele ya Wamisri wote,
4 ambao walikuwa wanawazika wazaliwa wao wa kwanza wa kiume aliowaua Mwenyezi-Mungu; kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa ameiadhibu hata miungu yao.
5 Basi, Waisraeli waliondoka Ramesesi, wakapiga kambi yao huko Sukothi.
6 Kutoka Sukothi, walipiga kambi yao huko Ethamu, ukingoni mwa jangwa.
7 Kutoka Ethamu, waligeuka na kurudi hadi Pi-hahirothi, mashariki ya Baal-sefoni, wakapiga kambi yao karibu na Migdoli.