1 “Mtu akiiba ng'ombe au kondoo na kumchinja au kumwuza, atatozwa ng'ombe watano kwa kila ng'ombe, na kondoo wanne kwa kila kondoo.
2 Mwizi akipatikana anavunja nyumba, akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya mauaji.
3 Lakini mwizi huyo akishikwa wakati jua limechomoza na kuuawa, aliyemuua atakuwa na hatia. Huyo mwizi anapaswa kulipa. Ikiwa hana kitu cha kulipa, basi, yeye mwenyewe atauzwa ili kulipia wizi wake.
4 Kama mnyama aliyeibiwa atapatikana kwa huyo mwizi akiwa hai, basi, mwizi atalipa mara mbili, awe ni ng'ombe, punda au kondoo.
5 “Mtu akiwalisha wanyama wake katika shamba la mizabibu au kumwachia mnyama wake kula katika shamba la mtu mwingine, atalipa hasara hiyo kwa mazao bora ya shamba lake mwenyewe au shamba lake la mizabibu.
6 “Mtu akiwasha moto nao ukachoma miti ya miiba na kusambaa hadi kuteketeza miganda ya nafaka, au nafaka ya mtu mwingine ambayo bado haijavunwa, au shamba lote likateketea, aliyewasha moto huo lazima alipe hasara hiyo yote.
7 “Mtu akimwachia mwenzake fedha au mali nyingine amtunzie, kisha ikaibiwa nyumbani mwake, mwizi akipatikana lazima alipe thamani yake mara mbili.