1 Hapo Yosefu akamkumbatia baba yake akilia na kumbusu.
2 Kisha, akawaagiza waganga wake wampake Israeli, baba yake, dawa ili asioze, nao wakafanya hivyo.
3 Kama kawaida, siku arubaini zilihitajika kwa kazi hiyo. Wamisri nao wakaomboleza kifo cha Yakobo kwa muda wa siku sabini.
4 Baada ya matanga kumalizika, Yosefu akawaambia watu wa jamaa ya Farao, “Ikiwa nimekubalika mbele yenu, tafadhali zungumzeni na Farao kwa niaba yangu kwamba baba yangu aliniapisha, akisema,
5 ‘Mimi karibu nitafariki. Yakupasa kunizika katika kaburi nililojichongea katika nchi ya Kanaani.’ Kwa hiyo namwomba aniruhusu niende kumzika baba yangu, kisha nitarudi.”
6 Farao akajibu, “Nenda ukamzike baba yako kama alivyokuapisha.”