7 Hakuna atakayemshirikisha aliyefiwa chakula cha kumfariji, wala kumpatia kinywaji cha kumfariji anywe kwa ajili ya kufiwa na mama au baba yake.
8 “Usiingie katika nyumba wanamofanya karamu. Usiketi kula na kunywa pamoja nao.
9 Maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nitazikomesha kabisa kutoka mahali hapa sauti za furaha na za shangwe, pamoja na sauti za bwana arusi na bibi arusi. Yote haya nitayafanya wakati wa uhai wenu mkiwa mnaona waziwazi.
10 Nawe utakapowaambia watu hao maneno haya yote, wao watakuuliza, ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ametamka uovu huu mkubwa dhidi yetu? Tumefanya kosa gani? Tumetenda dhambi gani dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu?’
11 Nawe utawajibu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wazee wenu waliniacha, wakaifuata miungu mingine, wakaitumikia na kuiabudu. Waliniacha, wala hawakuzitii sheria zangu.
12 Nyinyi mmefanya vibaya zaidi kuliko wazee wenu, maana kila mmoja wenu ni mkaidi na mwenye nia mbaya, wala hamnisikilizi.
13 Kwa hiyo, nitawatupilia mbali kutoka nchi hii mpaka kwenye nchi ambayo nyinyi wenyewe wala wazee wenu hawakuijua. Huko mtaitumikia miungu mingine usiku na mchana, wala sitawafadhili.