1 Neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu:
2 “Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Yaandike katika kitabu maneno yote niliyokuambia.
3 Maana siku zaja ambapo nitawarudishia fanaka zao watu wangu wa Israeli na Yuda na kuwarudisha katika nchi niliyowapa wazee wao, nao wataimiliki. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
4 Haya ndiyo mambo aliyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu watu wa Israeli na Yuda:
5 “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Kumesikika kilio cha hofusauti ya kutisha wala si ya amani.
6 Jiulizeni sasa na kufahamu:Je, mwanamume aweza kujifungua mtoto?Mbona basi, namwona kila mwanamumeamejishika kiunoni kama mwanamke mwenye utunguna nyuso zao zimegeuka rangi?
7 Kweli, siku hiyo ni kubwa,hakuna nyingine kama hiyo;ni siku ya huzuni kwa watu wa Yakobo;hata hivyo, wataokolewa humo.
8 “Siku hiyo itakapofika, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nitaivunja nira iliyo shingoni mwao na kukata minyororo yao.
9 Nao hawatakuwa tena watumwa wa wageni, bali watanitumikia mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, na mfalme wa ukoo wa Daudi ambaye nitawateulia.
10 “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Usiogope ee Yakobo mtumishi wangu,wala usifadhaike, ee Israeli;maana nitakuokoa huko mbali uliko,na wazawa wako kutoka uhamishoni.Utarudi na kuishi kwa amani,wala hakuna mtu atakayekuogopesha.
11 Maana mimi niko pamoja nawe, kukuokoa.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.Nitayaangamiza kabisa mataifa yote,ambayo nilikutawanya kati yao;lakini wewe sitakuangamiza kabisa.Nitakuadhibu kadiri unavyostahiliwala sitakuacha uende bila kukuadhibu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
12 “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Majeraha yako hayaponyeki,vidonda vyako havitibiki.
13 Hakuna atakayeshughulikia kisa chako,jeraha lako halina dawa,wewe hutaponyeshwa.
14 Wapenzi wako wote wamekusahau;hawajali chochote juu yako,nimekupiga pigo la adui;umeadhibiwa bila huruma,kwa kuwa kosa lako ni kubwa,dhambi zako ni nyingi mno.
15 Mbona unalia juu ya jeraha lako?Maumivu yako hayaponyeki.Nimekutendea hayo yote,kwa sababu kosa lako ni kubwa,dhambi zako ni nyingi mno.
16 Lakini wote wanaokuangamiza, wataangamizwa,na maadui zako wote watachukuliwa uhamishoni;wanaokuteka nyara, watatekwa nyara,wanaokuwinda nitawawinda.
17 “Nitakurudishia afya yako,na madonda yako nitayaponya,japo wamekuita ‘Aliyetupwa’,‘Mji Siyoni usio na wa kuutunza!’”
18 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Nitazirudisha tena fanaka za maskani ya Yakobo,na kuyaonea huruma makao yake;mji utajengwa upya juu ya magofu yake,na ikulu ya mfalme itasimama pale ilipokuwa.
19 Humo zitatoka nyimbo za shukranina sauti za wale wanaosherehekea.Nitawaongeza na wala hawatakuwa wachache;nitawafanya waheshimiwe wala hawatadharauliwa.
20 Watoto wao watakuwa kama walivyokuwa zamani,jumuiya yao itaimarika mbele yangu,nami nitawaadhibu wote wanaowakandamiza.
21 Kiongozi wao atakuwa mmoja wao,mtawala wao atatokea miongoni mwao.Nitamleta karibu naye atanikaribia;maana, nani anayethubutu kunikaribia kwa nguvu zake?Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
22 Nanyi mtakuwa watu wangu,nami nitakuwa Mungu wenu.”
23 Tazama, dhoruba kali kutoka kwa Mwenyezi-Mungu!Ghadhabu imezuka,kimbunga cha tufanikitamlipukia mtu mwovu kichwani.
24 Hasira ya Mwenyezi-Mungu haitarudi nyuma,mpaka atakapotekeleza na kukamilishamatakwa ya moyo wake.Siku zijazo mtayaelewa vema mambo hayo.