1 “Dhambi ya watu wa Yuda, imeandikwa kwa kalamu ya chuma; kwa ncha ya almasi imechorwa mioyoni mwao na katika pembe za madhabahu zao,
2 wakati watu wake wanakumbuka madhabahu zao na sanamu za mungu wa kike, Ashera, zilizowekwa kando ya miti mibichi juu ya vilele vya vilima,
3 na juu ya milima katika sehemu tambarare. Mali yenu na hazina zenu zote nitazitoa zitekwe nyara kulipia dhambi zenu mlizotenda kila mahali nchini mwenu.
4 Itawabidi muiachilie hiyo nchi yenu niliyowapeni, nami nitawafanya muwatumikie maadui zenu katika nchi msiyoijua, kwa sababu hasira yangu imewaka moto usiozimika milele.”
5 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Alaaniwe mtu anayemtegemea binadamu,mtu ambaye anategemea nguvu za binadamu,mtu ambaye moyo wake umeniacha mimi Mwenyezi-Mungu.
6 Huyo ni kama kichaka jangwani,hataona chochote chema kikimjia.Ataishi mahali pakavu nyikani,katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.
7 “Abarikiwe mtu anayemtegemea Mwenyezi-Mungu,mtu ambaye Mwenyezi-Mungu ndiye tegemeo lake.
8 Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya maji,upenyezao mizizi yake karibu na chemchemi.Hauogopi wakati wa joto ufikapo,majani yake hubaki mabichi.Hauhangaiki katika mwaka wa ukame,na hautaacha kuzaa matunda.
9 “Moyo wa mtu ni mdanganyifu kuliko vitu vyote;hauwezi kuponywa, hakuna awezaye kuuelewa!
10 Mimi Mwenyezi-Mungu hupima akilina kuchunguza mpaka ndani ya moyo wa mtu.Na hivyo humtendea kila mmoja,kulingana na mwenendo wake,kadiri ya matendo yake.”
11 Mtu apataye mali isiyo halalini kama kware akusanyaye makinda ambayo hakuyaangua:Wakati wa kilele cha ujana wake itamchopoka,na mwishoni atakuwa mtu mpumbavu.
12 Kuna kiti cha enzi kitukufukiti kilichoinuliwa juu;huko ndiko mahali petu patakatifu.
13 Ee Mwenyezi-Mungu tumaini la Israeli,wote wanaokukataa wataaibishwa;wanaokuacha wewe watatoweka,kama majina yaliyoandikwa vumbini,kwa maana wamekuacha wewe Mwenyezi-Mungu,uliye chemchemi ya maji ya uhai.
14 Uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nami nitapona;uniokoe, nami nitaokoka;maana, wewe ndiwe sifa yangu.
15 Tazama watu wanavyoniambia:“Jambo alilotishia Mwenyezi-Mungu liko wapi?Acha basi lije!”
16 Sikuikimbia huduma yako ya kuwa mchungajiwala sikutamani ile siku ya maafa ije.Wewe mwenyewe wajua nilichosema kwa mdomo wangu,nilichotamka wakijua waziwazi.
17 Usiwe tisho kwangu;wewe ndiwe kimbilio langu siku ya maafa.
18 Waaibishwe wale wanaonitesa,lakini mimi usiniache niaibike.Wafedheheshwe watu hao,lakini mimi usiniache nifedheheke.Uwaletee siku ya maafa,waangamize kwa maangamizi maradufu!
19 Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukasimame penye lango la watu ambapo wafalme wa Yuda huingia na kutoka mjini, na katika malango mengine yote ya Yerusalemu useme:
20 Sikieni neno la Mwenyezi-Mungu enyi wafalme wa Yuda, nanyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu ambao huingia kwa kupitia malango haya.
21 Waambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa usalama wa maisha yenu, muwe na hadhari msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, au kuingiza mzigo mjini kupitia malango ya Yerusalemu.
22 Msibebe mzigo kutoka majumbani mwenu siku ya Sabato wala kufanya kazi. Iadhimisheni siku ya Sabato kama siku takatifu kama nilivyowaamuru wazee wenu.
23 Lakini wazee wenu hawakunisikiliza wala kujali, bali walivifanya vichwa vyao kuwa vigumu, wakakataa kusikia na kufuata maagizo yangu.
24 “Lakini mkinisikiliza mimi Mwenyezi-Mungu, mkaacha kuingiza mzigo wowote kupitia malango ya mji huu siku ya Sabato, wala kufanya kazi siku hiyo,
25 basi, wafalme na wana wa wafalme wanaomfuata mfalme Daudi katika utawala, pamoja na watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, wataingia kwa kupitia malango ya mji huu, wakiwa wamepanda farasi na magari ya farasi. Nao mji huu utakuwa na watu daima.
26 Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na maeneo ya kandokando ya Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini, kutoka Shefela, kutoka nchi ya milima na kutoka Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na tambiko, sadaka za nafaka na ubani wa harufu nzuri, pamoja na matoleo ya shukrani. Vyote hivyo watavileta katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
27 Lakini msiponisikiliza na kuiadhimisha siku ya Sabato kama siku takatifu, msipoacha kubeba mizigo na kuingia nayo kupitia malango ya Yerusalemu siku ya Sabato, basi, nitawasha moto katika malango yake, nao utayateketeza majumba yote ya fahari ya Yerusalemu nao hautazimwa kamwe.”