Yeremia 5 BHN

Dhambi ya Yerusalemu

1 Kimbieni huko na huko mjini Yerusalemu;pelelezeni na kujionea wenyewe!Chunguzeni masoko yakemwone kama kuna mtu atendaye hakimtu atafutaye ukweli;akiwako, basi Mwenyezi-Mungu atausamehe Yerusalemu.

2 Ingawa wanaapa: “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo”,viapo vyao ni vya uongo.

3 Ee Mwenyezi-Mungu, wewe watafuta daima uaminifu.Umewatwanga, lakini hawakuona uchungu;umewateketeza, lakini walikataa kukosolewa.Wamezifanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko mwamba;wamekataa kabisa kurudi kwako.

4 Ndipo nilipowaza:“Hawa ni watu duni hawana akili;hawajui matakwa ya Mwenyezi-Mungu,hawajui Sheria ya Mungu wao.

5 Nitawaendea wakuu niongee nao;bila shaka, wao wanajua matakwa ya Mwenyezi-Mungu;wanajua sheria ya Mungu wao.”Lakini wote waliivunja nira yao.Waliikatilia mbali minyororo yao.

6 Kwa hiyo simba kutoka msituni atawaua;mbwamwitu kutoka jangwani atawararua.Chui anaivizia miji yao.Kila atokaye humo atararuliwa vipandevipande,kwa sababu dhambi zao ni nyingi,maasi yao ni makubwa.

7 Mwenyezi-Mungu anauliza:“Nitawezaje kukusamehe ee Yerusalemu?Watu wako wameniasi;wameapa kwa miungu ya uongo.Nilipowashibisha kwa chakula,wao walifanya uzinzi,wakajumuika majumbani mwa makahaba.

8 Walikuwa kama farasi walioshiba wenye tamaa,kila mmoja akimtamani mke wa jirani yake.

9 Je, nisiwaadhibu kwa mambo haya yote?Nisilipize kisasi juu ya taifa kama hili?

10 “Pandeni mpite katika mashamba yake ya mizabibumkaharibu kila kitu bila kumaliza kabisa.Yakateni matawi yake,kwani hayo si yangu mimi Mwenyezi-Mungu.

11 Naam, watu wa Israeli na watu wa Yuda,wamekosa kabisa uaminifu kwangu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Matokeo ya kuachwa na Mungu

12 Wamesema uongo juu ya Mwenyezi-Munguwamesema: “Hatafanya kitu;hatutapatwa na uovu wowote;hatutashambuliwa wala kuona njaa.

13 Manabii si kitu, ni upepo tu;maana neno lake Mungu halimo ndani yao.”Basi hayo na yawapate wao wenyewe!

14 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:“Kwa kuwa wao wamesema jambo hilo,sasa nitayafanya maneno niliyokupa wewe Yeremia kuwa moto.Watu hawa watakuwa kuni,na moto huo utawateketeza.

15 “Nami Mwenyezi-Mungu nasema juu yenu enyi Waisraeli:Mimi naleta taifa moja kutoka mbali,lije kuwashambulia.Taifa ambalo halishindiki,taifa ambalo ni la zamani,ambalo lugha yake hamuifahamu,wala hamwezi kuelewa wasemacho.

16 Mishale yao husambaza kifo;wote ni mashujaa wa vita.

17 Watayala mazao yenu na chakula chenu;watawamaliza watoto wenu wa kike na wa kiume.Watachinja makundi yenu ya kondoo na ng'ombe;wataiharibu mizabibu yenu na mitini yenu.Miji yenu ya ngome mnayoitegemea,wataiharibu kwa silaha zao.

18 “Lakini, hata katika siku hizo mimi Mwenyezi-Mungu nasema, sitawaangamiza na kuwamaliza kabisa.

19 Na watu wenu watakapouliza ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametutendea mambo hayo yote?’ Wewe utawaambia, ‘Nyinyi mlimwacha Mwenyezi-Mungu, mkaitumikia miungu ya kigeni katika nchi yenu. Basi ndivyo mtakavyowatumikia watu wengine katika nchi isiyo yenu.’

Mungu awaonya watu wake

20 “Watangazie wazawa wa Yakobo,waambie watu wa Yuda hivi:

21 Sikilizeni enyi wajinga na wapumbavu;watu mlio na macho, lakini hamwoni,mlio na masikio, lakini hamsikii.

22 Mbona hamniogopi? Nauliza mimi Mwenyezi-Mungu!Kwa nini hamtetemeki mbele yangu?Mimi niliweka mchanga uwe mpaka wa bahari,kizuizi cha daima ambacho bahari haiwezi kuvuka.Ingawa mawimbi yanaupiga, hayawezi kuupita;ingawa yananguruma, hayawezi kuuruka.

23 Lakini watu hawa wana moyo wa ukaidi na uasi;wameniacha wakaenda zao.

24 Wala hawasemi mioyoni mwao;‘Na tumche Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,anayetujalia mvua kwa wakati wake,anayetupatia mvua za masika na mvua za vuli;na kutupa majira maalumu ya mavuno.’

25 Makosa yenu yamewazuia msipate baraka hizo,dhambi zenu zimewafanya msipate mema.

26 Naam, kuna walaghai miongoni mwa watu wangu,watu ambao hunyakua mali za wengine.Wako kama wawindaji wa ndege:Hutega mitego yao na kuwanasa watu.

27 Kama vile kapu lililojaa ndege walionaswa,ndivyo nyumba zao zilivyojaa mali za udanganyifu.Ndiyo maana wamekuwa watu wakubwa na matajiri,

28 wamenenepa na kunawiri.Katika kutenda maovu hawana kikomohawahukumu yatima kwa haki wapate kufanikiwa,wala hawatetei haki za watu maskini.

29 “Je, nisiwaadhibu kwa mambo haya?Je nitaacha kulipiza kisasi taifa kama hili?

30 Jambo la ajabu na la kuchukizalimetokea katika nchi hii:

31 Manabii wanatabiri mambo ya uongo,makuhani nao hutafuta faida yao wenyewe;na watu wangu wanaona jambo hilo kuwa sawa. Lakini mwisho utakapofika mtafanyaje?”