Yeremia 23 BHN

Tumaini la baadaye

1 “Ole wao wachungaji wanaowaangamiza na kuwatawanya kondoo wa malisho yangu!”

2 Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli nasema hivi kuhusu wachungaji wanaowachunga watu wangu: Nyinyi mmewatawanya kondoo wangu na kuwafukuza, wala hamkuwatunza. Basi, nami pia nitawaadhibu kwa ajili ya matendo yenu maovu.

3 Kisha, nitawakusanya kondoo wangu waliobaki kutoka nchi zote nilikowatawanya, na kuwarudisha malishoni mwao. Nao watazaa na kuongezeka.

4 Nitawapa wachungaji watakaowatunza vema, nao hawatakuwa na woga tena wala kufadhaika, na hakuna hata mmoja wao atakayepotea, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

5 “Tazama, siku zaja nitakapomchipushia Daudi chipukizi adili. Huyo atatawala kama mfalme, na atatenda kwa busara, haki na uadilifu katika nchi.

6 Katika siku za utawala wake, Yuda ataokolewa na Israeli ataishi kwa usalama. Naye ataitwa, ‘Mwenyezi-Mungu ni uadilifu wetu.’

7 “Kwa hiyo siku zaja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, ambapo watu hawataapa tena kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyewatoa watu wa Israeli nchini Misri’,

8 bali wataapa kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyewatoa na kuwaongoza Waisraeli kutoka nchi ya kaskazini na kutoka nchi zote ambako aliwatawanya.’ Kisha wataishi katika nchi yao wenyewe.”

Manabii wabaya

9 Kuhusu hao manabii wasiofaa,mimi imevunjika moyo,mifupa yangu yote inatetemeka;nimekuwa kama mlevi,kama mtu aliyelemewa na pombe,kwa sababu yake Mwenyezi-Munguna maneno yake matakatifu.

10 Maana, nchi imejaa wazinzi;kwa sababu ya laana, nchi inaomboleza,na malisho ya nyanda zake yamekauka.Mienendo ya watu ni miovu,nguvu zao zinatumika isivyo halali.

11 Mwenyezi-Mungu asema:“Manabii na makuhani, wote hawamchi Mungu,uovu wao nimeuona hata nyumbani mwangu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

12 Kwa hiyo njia zao zitakuwa vichochoro vya utelezi gizaniambamo watasukumwa na kuanguka;maana, nitawaletea maafa,ufikapo mwaka wa kuwaadhibu,Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

13 “Miongoni mwa manabii wa Samaria,nimeona jambo la kuchukiza sana:Walitabiri kwa jina la Baaliwakawapotosha watu wangu Waisraeli.

14 Lakini miongoni mwa manabii wa Yerusalemu,nimeona kinyaa cha kutisha zaidi:Wanafanya uzinzi na kusema uongo;wanawaunga mkono wanaotenda maovuhata pasiwe na mtu anayeachana na uovu.Kwangu wote wamekuwa kama watu wa Sodoma;wakazi wake wamekuwa wabaya kama watu wa Gomora.

15 “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi juu ya manabii wa Yerusalemu:Nitawalisha uchungu,na kuwapa maji yenye sumu wanywe.Maana, kutoka kwa manabii wa Yerusalemukutomcha Mungu kumeenea kila mahali nchini.”

16 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Msisikilize maneno ya manabii wanaowatabiria; wanawapeni matumaini ya uongo. Wanayowaambia ni maono yao wenyewe, wala hayakutoka kwangu mimi Mwenyezi-Mungu.

17 Wao hawakomi kuwaambia wale wanaodharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu: ‘Mambo yatawaendea vema.’ Na kumwambia kila mtu afuataye kwa ukaidi fikira zake; ‘Hakuna baya lolote litakalokupata!’”

18 Lakini, ni yupi kati ya manabii haoaliyepata kuhudhuria baraza la Mwenyezi-Mungu,hata akasikia na kuelewa neno lake?Au ni nani aliyejali neno lake,hata akapata kulitangaza?

19 Tazama, dhoruba kutoka kwa Mwenyezi-Mungu!Ghadhabu imezuka;kimbunga cha tufanikitamlipukia mtu mwovu kichwani.

20 Hasira ya Mwenyezi-Mungu haitarudi nyuma,mpaka atakapotekeleza na kukamilishamatakwa ya moyo wake.Siku zijazo mtayaelewa vema mambo hayo.

21 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Mimi sikuwatuma hao manabii,lakini wao walikwenda mbio;sikuwaambia kitu chochote,lakini wao walitabiri!

22 Kama wangalihudhuria baraza langu,wangaliwatangazia watu wangu maneno yangu,wakawageuza kutoka katika njia zao mbovu,na kutoka katika matendo yao maovu.

23 “Mimi ni Mungu aliye karibu, si Mungu aliye mbali.

24 Je, mtu aweza kujificha mahali pa siri hata nisiweze kumwona? Hamjui kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nipo kila mahali, mbinguni na duniani? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

25 Mimi nimeyasikia maneno waliyosema hao manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, ‘Nimeota ndoto, nimeota ndoto!’

26 Itakuwa hivyo mpaka lini? Hao manabii wataendelea mpaka lini kupotoka moyo; kutabiri uongo na udanganyifu wa mioyo yao wenyewe?

27 Kwa ndoto zao hizo wanapanga kuwafanya watu wangu wanisahau mimi kama baba zao walivyonisahau, wakamwendea Baali!

28 Nabii aliyeota ndoto, na aitangaze ndoto yake, lakini yeye aliye na neno langu, na alitangaze kwa uaminifu. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema, makapi si sawa na ngano!

29 Neno langu ni kama moto; ni kama nyundo ipasuayo miamba vipandevipande.

30 Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nitawashambulia manabii ambao wanaibiana maneno yangu.

31 Kweli mimi Mwenyezi-Mungu nasema, nitawashambulia manabii wanaoropoka maneno yao wenyewe na kusema, ‘Mwenyezi-Mungu asema’.

32 Naam, mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa nitawashambulia manabii wanaotabiri ndoto zao za uongo kwa watu wangu, na kuwapotosha kwa uongo wao na kuropoka kwao. Mimi sikuwatuma wala kuwaamuru waende; kwa hiyo hawatawafaa watu hao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Neno la Mwenyezi-Mungu ni mzigo?

33 Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Mtu yeyote, awe nabii au kuhani, akikuuliza: ‘Uko wapi mzigo anaotubebesha Mwenyezi-Mungu?’ Wewe utawaambia: ‘Nyinyi ndio mzigo kwa Mwenyezi-Mungu naye atawatupa mbali.’

34 Tena nabii au kuhani, au mtu yeyote atakayesema ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ nitamwadhibu pamoja na jamaa yake yote.

35 Kitu mnachopaswa kuulizana nyinyi kwa nyinyi ni ‘Mwenyezi-Mungu amejibu nini?’ au, ‘Mwenyezi-Mungu amesema nini?’

36 Lakini jambo la ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ msilitaje tena. Kile anachosema binadamu ni mzigo kwake mwenyewe. Watu wanayapotosha maneno ya Mungu aliye hai, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao.

37 Basi mtamwuliza nabii hivi: ‘Mwenyezi-Mungu amekujibu nini?’ au, ‘Mwenyezi-Mungu amesema nini?’

38 Lakini wao wakivunja amri yangu na kusema, ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ wakati ambapo mimi niliwakataza wasiseme, ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ basi, waambie kuwa

39 mimi nitawanyanyua na kuwatupilia mbali, wao wenyewe pamoja na mji niliowapa wao na wazee wao.

40 Nitawaletea fedheha ya milele na aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”