1 Hili ni neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, wakati mfalme Sedekia alipowatuma Pashuri mwana wa Malkia, na kuhani Sefania mwana wa Maaseya, wamwambie Yeremia hivi:
2 “Tafadhali, tuombee kwa Mwenyezi-Mungu maana Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, anaanza vita dhidi yetu. Labda Mwenyezi-Mungu atatufanyia mwujiza kama afanyavyo mara kwa mara na kumfanya Nebukadneza atuache na kwenda zake.”
3 Yeremia akawaambia:
4 Nendeni mkamwambie Sedekia kwamba hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: “Sedekia! Nitakugeuzia wewe mwenyewe silaha unazotumia kupigana na mfalme wa Babuloni na Wakaldayo wanaowazingira nje ya kuta za mji. Nitazikusanya silaha zote katikati ya mji huu.
5 Mimi mwenyewe nitapigana nawe kwa mkono ulionyoka na wenye nguvu, kwa hasira, ukali na ghadhabu kubwa.
6 Nitawaua wakazi wa mji huu: Binadamu na wanyama kadhalika. Watakufa kwa maradhi mabaya sana.
7 Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa, baadaye wewe Sedekia mfalme wa Yuda, watumishi wako na watu wa mji huu ambao mtaponea maradhi hayo mabaya pamoja na vita na njaa, nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni na mikononi mwa adui zenu wanaowawinda. Nebukadneza atawaua kwa upanga na wala hatawahurumia au kuwaachilia au kuwasamehe. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
8 “Nawe Yeremia utawaambia watu hawa kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sikilizeni! Mimi nawapeni nafasi ya kuchagua njia ya uhai au njia ya kifo.
9 Mtu atakayebaki mjini humu atauawa kwa upanga au kwa njaa au kwa maradhi mabaya. Lakini mtu atakayetoka nje ya mji na kujisalimisha kwa Wakaldayo wanaouzingira mji, ataishi; naam, atayanusurisha maisha yake.
10 Nimeamua kuuletea mji huu maafa na sio mema, nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Nitautia mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteketeza kwa moto.
11 “Utaiambia jamaa ya mfalme wa Yuda: Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu,
12 enyi jamaa ya Daudi! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Tekelezeni haki tangu asubuhi,na kuwakomboa mikononi mwa wadhalimuwote walionyanganywa mali zao.La sivyo, hasira yangu itachomoza kama moto,itawaka na wala hakuna atakayeweza kuizima,kwa sababu ya matendo yenu maovu.
13 Tazama, mimi sasa napambana nanyi mnaoishi bondeni,mnaokaa kwenye mwamba wa tambarare,nyinyi mnaosema, ‘Nani atathubutu kutushambulia?Nani awezaye kuingia katika makazi yetu?’
14 Nitawaadhibu kadiri ya matendo yenu;mimi Mwenyezi-Mungu nasema.Nitawasha moto katika msitu wenunao utateketeza kila kitu kinachouzunguka.”