1 Neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kwa njia ya nabii Yeremia kuhusu nchi ya Babuloni na nchi ya Wakaldayo:
2 “Tangazeni kati ya mataifa,twekeni bendera na kutangaza,Msifiche lolote. Semeni:‘Babuloni umetekwa,Beli ameaibishwa.Merodaki amefadhaishwa;sanamu zake zimeaibishwa,vinyago vyake vimefadhaishwa.’
3 “Kwa maana, taifa kutoka kaskazini limefika kuushambulia; litaifanya nchi yake kuwa uharibifu. Hakuna atakeyeishi humo; watu na wanyama watakimbia mbali.
4 “Siku hizo na wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, watu wa Israeli na watu wa Yuda watakusanyika pamoja na kurudi wakilia huku wananitafuta mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
5 Watauliza njia ya kwenda Siyoni, huku nyuso zao zimeelekea huko, wakisema, ‘Njoni!’ Nao watajiunga na Mwenyezi-Mungu katika agano la milele ambalo kamwe halitasahauliwa.
6 “Watu wangu walikuwa kondoo waliopotea; wachungaji wao wamewapotosha, wakawageuza kuelekea milimani; walitembea toka mlima hadi kilima, wakasahau zizi lao.
7 Watu wote waliowakuta waliwaua, na maadui zao wamesema, ‘Hatuna hatia sisi’, maana hao wamemkosea Mwenyezi-Mungu aliye malisho yao ya kweli; Mwenyezi-Mungu ambaye ni tegemeo la wazee wao!
8 “Kimbieni kutoka Babuloni! Tokeni nje ya nchi ya Wakaldayo, muwe kama mabeberu mbele ya kundi.
9 Maana, mimi nitachochea mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini washambulie Babuloni. Watajiandaa kuishambulia Babuloni na kuiteka. Mishale yao ni kama shujaa hodari asiyerudi mikono mitupu.
10 Nchi ya Wakaldayo itaporwa, na hao watakaoipora wataridhika. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
11 “Enyi waporaji wa mali yangu!Japo mnafurahi na kushangilia,mnarukaruka kama mtamba wa ng'ombe anayepura nafaka,na kulia kama farasi dume,
12 nchi yenu ya kuzaliwa itaaibishwa;hiyo nchi mama yenu itafedheheshwa.Lo! Babuloni itakuwa ya mwisho kati ya mataifa,itakuwa nyika kame na jangwa.
13 Kwa sababu ya ghadhabu yangu Mwenyezi-Mungu,Babuloni haitakaliwa kabisa na watu,bali itakuwa jangwa kabisa;kila atakayepita karibu nayo atashangaaataizomea kwa sababu ya majeraha yake.
14 “Enyi nyote wapiga mishale stadi,shikeni nafasi zenu kuuzingira mji wa Babuloni;upigeni, msibakize mshale hata mmoja,maana umenikosea mimi Mwenyezi-Mungu.
15 Upigieni kelele za vita pande zote,sasa Babuloni umejitoa ukamatwe.Ngome zake zimeanguka,kuta zake zimebomolewa.Ninalipiza kisasi juu ya BabuloniBasi jilipizeni kisasi,utendeeni kama ulivyowatenda wengine.
16 Zuieni watu wasipande mbegu Babuloni,wala wasivune wakati wa mavuno.Kutokana na upanga wa udhalimu,kila mmoja atawarudia watu wakekila mmoja atakimbilia nchini mwake.
17 “Israeli ni kondoo wanaowindwa na kufukuzwa na simba. Kwanza waliangamizwa na mfalme wa Ashuru, na sasa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, amevunjavunja mifupa yake.
18 Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nitamwadhibu mfalme wa Babuloni na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.
19 Nitawarudisha Waisraeli nchini mwao, nao watakula mavuno yatakayolimwa juu ya mlima Karmeli na Bashani na watatosheka kwa chakula kutoka milima ya Efraimu na Gileadi.
20 Siku hizo na wakati huo, uovu utatafutwa nchini Israeli, lakini hautapatikana; dhambi itatafutwa nchini Yuda, lakini haitapatikana; maana mimi nitawasamehe wale ambao nimewabakiza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21 “Pandeni, mwiendee nchi ya Merathaimu,nendeni kuishambulia;washambulieni wakazi wa Pekodina kuwaangamiza kabisa watu wake.Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.Fanyeni kila kitu nilichowaamuru.
22 Kelele za vita zinasikika nchini,kuna uharibifu mkubwa.
23 Jinsi gani huo mji uliokuwa nyundo ya dunia nzimaunavyoangushwa chini na kuvunjika!Babuloni umekuwa kinyaamiongoni mwa mataifa!
24 Ewe Babuloni, nilikutegea mtego ukanaswa,wala hukujua juu yake;ulipatikana, ukakamatwa,kwa sababu ulishindana nami Mwenyezi-Mungu.
25 Nimefungua ghala yangu ya silaha,nikatoa humo silaha za ghadhabu yangu,maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshinina kazi ya kufanyakatika nchi ya Wakaldayo.
26 Njoni mkamshambulie kutoka kila upande;zifungueni ghala zake za chakula;mrundikieni marundo ya nafaka!Iangamizeni kabisa nchi hii;msibakize chochote!
27 Waueni askari wake hodari;waache washukie machinjoni.Ole wao, maana siku yao imewadia,wakati wao wa kuadhibiwa umefika.
28 “Sikiliza! Wakimbizi na watoro kutoka nchi ya Babuloni wanakuja kutangaza huko Siyoni jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyolipiza kisasi kwa ajili ya hekalu lake.
29 “Waiteni wapiga mishale waishambulie Babuloni. Pelekeni kila mtu ajuaye kuvuta upinde. Uzingireni mji pasiwe na yeyote atakayetoroka. Ulipizeni kadiri ya matendo yake yote; utendeeni kama ulivyowatendea wengine, maana kwa kiburi ulinidharau mimi Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli.
30 Kwa hiyo, vijana wake watauawa katika mitaa yake, na majeshi yake yote yataangamizwa siku hiyo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
31 “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi,napigana nawe ewe mwenye kiburi,maana siku yako ya adhabu imefika,wakati nitakapokuadhibu umewadia.
32 Mwenye kiburi atajikwaa na kuanguka,wala hapatakuwa na mtu wa kumwinua.Nitawasha moto katika miji yake,nao utateketeza kila kitu kandokando yake.”
33 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Watu wa Israeli wanakandamizwa; hali kadhalika na watu wa Yuda. Wale waliowachukua mateka wamewabana sana na wanakataa kuwaachia.
34 Lakini mimi, Mkombozi wao ni mwenye nguvu. Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina langu. Hakika nitatetea kisa chao ili nilete amani katika nchi yao, lakini taabu kwa wakazi wa Babuloni.
35 “Kifo kwa Wakaldayo,kwa wakazi wa Babulonina maofisa na wenye hekima wake!
36 Kifo kwa waaguzi,wanachotangaza ni upumbavu tu!Kifo kwa mashujaa wake,ili waangamizwe!
37 Kifo kwa farasi wake na uharibifu kwa magari yake,kifo kwa majeshi yake yote ya kukodiwa,ili wawe na woga kama wanawake!Uharibifu kwa hazina zake zoteili zipate kuporwa.
38 Ukame uyapate majiili yapate kukauka!Maana Babuloni ni nchi ya sanamu za miungu,watu ni wendawazimu juu ya vinyago vyao.
39 “Kwa hiyo wanyama wa porini, mbwamwitu pamoja na mbuni, watakaa Babuloni. Hapatakaliwa kamwe na watu vizazi vyote vijavyo.
40 Kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyoiangamiza miji ya Sodoma na Gomora na miji ya jirani, vivyo hivyo hapatakuwa na mtu yeyote atakayeishi humo. Naam, hakuna mtu yeyote atakeyekaa huko. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
41 “Tazama! Watu wanakuja kutoka kaskazini;taifa lenye nguvu na wafalme wengiwanajitayarisha kutoka miisho ya dunia.
42 Wameshika pinde zao na mikuki;ni watu wakatili na wasio na huruma.Vishindo vyao ni kama mvumo wa bahari,wamepanda farasi.Wamejipanga tayari kwa vita,dhidi yako wewe Babuloni!
43 Mfalme wa Babuloni amesikia habari zao,nayo mikono yake ikawa kama kamba.Ameshikwa na dhiki na uchungu kama mama anayejifungua.
44 “Tazama, mimi nitakuwa kama simba anayechomoza kutoka msitu wa mto Yordani na kuingia kwenye malisho mazuri: Mimi Mwenyezi-Mungu nitawafukuza ghafla watu wake kutoka kwake. Nami nitamweka huko kiongozi yeyote nitakayemchagua. Maana, ni nani anayeweza kulinganishwa nami? Nani awezaye kunishtaki? Ni mchungaji gani awezaye kunipinga?
45 Kwa hiyo, sikilizeni mpango ambao mimi Mwenyezi-Mungu nimepanga dhidi ya Babuloni pamoja na mambo niliyokusudia kuitendea nchi ya Wakaldayo: Hakika watoto wao wataburutwa na kuchukuliwa; kweli kutakuwa na mshangao mkubwa katika makao yao.
46 Kwa kishindo cha kutekwa kwa Babuloni dunia itatetemeka, na kilio chake kitasikika miongoni mwa mataifa mengine.”