1 “Mume akimpa talaka mkewe,naye akaondoka kwake,na kuwa mke wa mwanamume mwingine,je mume yule aweza kumrudia mwanamke huyo?Je, kufanya hivyo hakutaitia nchi unajisi mkubwa?Wewe Israeli, umefanya ukahaba na wapenzi wengi,je, sasa unataka kunirudia mimi?
2 Inua macho uvitazame vilele vya vilima!Pako wapi mahali ambapo hawajalala nawe?Uliwangoja wapenzi wako kando ya njia,kama bedui aviziavyo watu jangwani.Umeifanya nchi kuwa najisi,kwa ukahaba wako mbaya kupindukia.
3 Ndiyo maana manyunyu yamezuiliwa,na wala mvua za vuli hazijanyesha.Hata hivyo uko macho makavu kama kahaba,huna haya hata kidogo.
4 “Hivi punde tu si ulinililia ukisema:‘Wewe u baba yangu,ulinipenda tangu utoto wangu?
5 Je, utanikasirikia daima?Utachukizwa nami milele?’Israeli, hivyo ndivyo unavyosema;na kumbe umetenda uovu wote ulioweza.”
6 Wakati wa utawala wa mfalme Yosia, Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Je, umeona jinsi Israeli asiye mwaminifu alivyofanya? Aliniacha, akapanda juu ya kila kilima kirefu na kwenda chini ya kila mti wenye majani mabichi, akafanya ukahaba wake humo!
7 Mimi nilidhani kuwa baada ya kufanya yote hayo, atanirudia. Lakini wapi; hakunirudia. Yuda, dada yake mdanganyifu, alishuhudia yote hayo.
8 Zaidi ya hayo, Yuda alishuhudia kuwa nilimpa Israeli talaka kwa sababu ya ukahaba wake na kwa kukosa uaminifu kwangu. Lakini hata hivyo, Yuda, dada yake mdanganyifu, hakuogopa; naye pia alikwenda na kufanya ukahaba!
9 Na, kwa kuwa yeye aliona kuwa ukahaba ni jambo dogo sana kwake, aliitia nchi unajisi, na kufanya ukahaba kwa kuabudu mawe na miti.
10 Pamoja na hayo yote, Yuda, dada mdanganyifu wa Israeli, hakunirudia kwa moyo wote, bali kwa unafiki tu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
11 Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Mwasi Israeli amedhihirisha kuwa yeye ni afadhali kuliko Yuda mdanganyifu.
12 Basi, nenda ukamtangazie Israeli maneno yafuatayo:Rudi, ewe Israeli, usiye mwaminifu.Nami sitakutazama kwa hasirakwa kuwa mimi ni mwenye huruma.Naam, sitakukasirikia milele.
13 Wewe, kiri tu kosa lako:Kwamba umeniasi mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako;kwamba chini ya kila mti wenye majani,umewapa miungu wengine mapenzi yakowala hukuitii sauti yangu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
14 “Rudini, enyi watoto msio na uaminifu,maana, mimi ndimi Bwana wenu.Nitawachukua mmoja kutoka kila mji,na wawili kutoka katika kila ukoo,niwapeleke hadi mlimani Siyoni.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
15 “Nitawapeni wachungaji wanipendao moyoni, watakaowalisha kwa maarifa na busara.
16 Siku hizo, wakati mtakapokuwa mmeongezeka na kuwa wengi nchini, watu hawatalitajataja tena sanduku langu la agano. Hawatalifikiria kabisa, wala hawatalikumbuka tena; hawatalihitaji, wala hawataunda jingine.
17 Wakati huo, mji wa Yerusalemu utaitwa ‘Kiti cha Enzi cha Mwenyezi-Mungu’, na mataifa yote yatakusanyika humo mbele yangu. Hawatafuata tena ukaidi wa matendo yao.
18 Siku hizo, watu wa Yuda wataungana na watu wa Israeli, na wote kwa pamoja watatoka katika nchi ya kaskazini na kurudi katika nchi niliyowapa wazee wenu iwe mali yao.”
19 Mwenyezi-Mungu asema,“Israeli, mimi niliwaza,laiti ningekuweka miongoni mwa wanangu,na kukupa nchi nzuri ajabu,urithi usio na kifani kati ya mataifa yote.Nilidhani ungeniita, ‘Baba Yangu’,na kamwe usingeacha kunifuata.
20 Lakini kama mke asiye mwaminifu amwachavyo mumewe,ndivyo ulivyokosa uaminifu kwangu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21 “Kelele zasikika juu ya vilima:Waisraeli wanalia na kuomboleza,kwa kuwa wamepotoka katika njia zao,wamenisahau mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
22 Rudini, enyi watoto msio na uaminifu,mimi nitaponya utovu wenu wa uaminifu.“Nanyi mwasema: ‘Tazama, sisi tunarudi kwako,maana, wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
23 Kweli tumedanganyika mno kuabudu huko vilimani,hakika wokovu wa Israeliwatoka kwake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
24 “ ‘Tangu ujana wetu, tendo hili la aibu limeangamiza kila kitu walichotolea jasho wazee wetu: Makundi yao ya kondoo na ng'ombe, wana wao na binti zao.
25 Hatuna budi kujilaza chini kwa aibu, na kuiacha fedheha yetu itufunike. Tangu ujana wetu hadi leo hii, wazee wetu na sisi wenyewe tumetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala hatukumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’”