1 Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi:“Ole watu wa Nebo, maana mji wake umeharibiwa!Kiriathaimu umeaibishwa, umetekwa,ngome yake imebomolewa mbali;
2 fahari ya Moabu imetoweka.Mpango ulifanywa huko Heshboni dhidi yake:‘Haya! Tuwaangamize wasiwe tena taifa!’Nawe Madmeni utanyamazishwa,upanga utakufuatia.
3 Sikiliza! Kilio kutoka Horonaimu:‘Maangamizi na uharibifu mkubwa!’
4 Moabu tayari imeangamizwakilio chake chasikika mpaka Soari.
5 Walionusurika wanapanda kwenda Luhithihuku wanalia kwa sauti.Wanapoteremka kwenda Horonaimu,wanasikia kilio cha uharibifu.
6 Kimbieni! Jiokoeni wenyewe!Kimbieni kama pundamwitu jangwani!
7 “Moabu, ulitumainia ngome na hazina zako,lakini sasa wewe pia utatekwa;mungu wako Kemoshi atapelekwa uhamishonipamoja na makuhani na watumishi wake.
8 Mwangamizi atapita katika kila mji,hakuna mji utakaomwepa;kila kitu mabondeni kitaangamianyanda za juu zitaharibiwa,kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.
9 Mchimbieni Moabu kaburi,maana kuangamia kwake ni hakika;miji yake itakuwa tupu,bila mkazi hata mmoja.
10 Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Mwenyezi-Mungu kwa ulegevu; alaaniwe anayezuia upanga wake usimwage damu!
11 Moabu amestarehe tangu ujana wake,ametulia kama divai katika gudulia.Hajamiminiwa toka chombo hata chombo,hajapata kuchukuliwa uhamishoni.Kwa hiyo yungali na ladha yake,harufu yake nzuri haijabadilika kamwe.
12 “Kwa hiyo, wakati waja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu ambapo nitampelekea wamiminaji ambao wataimimina divai yake. Wataimwaga yote kutoka vyombo vyake na kuvivunja vipandevipande.
13 Hapo Wamoabu watamwonea aibu mungu wao Kemoshi, kama vile watu wa Israeli walivyomwonea aibu Betheli, mungu waliyemtegemea.
14 Mwawezaje kusema: ‘Sisi ni mashujaa,na watu wenye nguvu nyingi za vita?’
15 Mwangamizi wa Moabu na miji yake amewasilivijana wake wazuri wamechinjwa.Nimesema mimi mfalmeniitwaye Mwenyezi-Mungu wa Majeshi.
16 Janga la Moabu limekaribia,maangamizi yake yanawasili haraka.
17 Mwomboleezeni Moabu, enyi jirani zake wote,na nyote mnaomjua vizurisemeni: ‘Jinsi gani fimbo ya nguvu ilivyovunjwa,naam fimbo ile ya fahari!’
18 Enyi wenyeji wa Diboni:Shukeni kutoka mahali penu pa fahari,mkaketi katika ardhi isiyo na maji.Maana mwangamizi wa Moabu,amefika kuwashambulia;amekwisha haribu ngome zenu.
19 Enyi wakazi wa Aroeri,simameni kando ya njia mtazame!Mwulizeni anayekimbia na anayetoroka:‘Kumetokea nini?’
20 Moabu imeaibishwa maana imevunjwa;ombolezeni na kulia.Tangazeni kando ya mto Arnoni,kwamba Moabu imeharibiwa kabisa.
21 “Hukumu imeifikia miji iliyo nyanda za juu: Holoni, Yasa, Mefaathi,
22 Diboni, Nebo, Beth-diblathaimu,
23 Kiriathaimu, Beth-gamuli, Beth-meoni,
24 Keriothi na Bosra. Naam, hukumu imeifikia miji yote ya Moabu mbali na karibu.
25 Nguvu za Moabu zimevunjiliwa mbali na uwezo wake umevunjwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
26 “Mlewesheni Moabu kwa sababu alijikuza dhidi yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Moabu atagaagaa katika matapishi yake na watu watamcheka.
27 Kumbuka Moabu ulivyomcheka Israeli. Je, alikamatwa pamoja na wezi, hata ukawa unatikisa kichwa chako kila ulipoongea juu yake?
28 “Enyi wenyeji wa Moabu,tokeni mijini, mkakae mapangoni!Mwigeni njiwa ajengaye kiota penye genge.
29 Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu;Moabu ana majivuno sana.Tumesikia juu ya kujiona, kiburi na majivuno yake;tumesikia jinsi anavyojigamba moyoni.
30 “Nami Mwenyezi-Mungu nasema:Najua ufidhuli wake;Majivuno yake ni ya bure,na matendo yake si kitu.
31 Kwa hiyo ninaomboleza juu ya Moabu,ninalia kwa ajili ya Wamoabu wote,naomboleza juu ya watu wa Kir-heresi.
32 Nakulilia wewe bustani ya Sibmakuliko hata watu wa Yazeri.Matawi yako yametandampaka ngambo ya bahari ya Chumviyakafika hata mpaka Yazeri.Lakini mwangamizi ameyakumbamatunda yako ya kiangazi na zabibu zako.
33 Furaha na shangwe zimeondolewakutoka nchi ya Moabu yenye rutuba.Nimeikomesha divai kutoka mashinikizohakuna mtu anayekamua zabibu kwa shangwe;kelele zinazosikika si za shangwe.
34 “Kilio cha watu wa Heshboni chasikika huko Eleale mpaka Yahazi; kinaenea kutoka Soari mpaka Horonaimu na hata Eglath-shelishiya. Hata maji ya kijito Nimrimu yamekauka.
35 Nami nitamfutilia mbali kila mtu katika Moabu ambaye anatambikia vilimani na kumfukizia ubani mungu wake.
36 “Kwa hiyo, moyo wangu unaomboleza juu ya watu wa Moabu na watu wa Kir-heresi, kama mpiga zumari mazishini; maana hata mali yote waliyojipatia imeangamia.
37 Kila mtu amenyoa upara na ndevu zake. Wote wamejikatakata mikononi na viunoni wamevaa mavazi ya gunia.
38 Juu ya nyumba za Moabu na katika viwanja vyao hakuna kinachosikika ila tu maombolezo. Mimi nimemvunja Moabu kama chombo kisichotakiwa na mtu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
39 Tazama alivyovunjika! Tazama wanavyoomboleza! Ajabu jinsi Moabu alivyorudi nyuma kwa aibu! Moabu amekuwa kichekesho na kioja kwa jirani zake wote.”
40 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Tazama, taifa litaruka kasi kuivamia Moabu,kama tai aliyekunjua mabawa yake.
41 Miji yake itatekwa,ngome zitachukuliwa.Siku hiyo mioyo ya wanajeshi wa Moabu,itaogopa kama mwanamke anayejifungua.
42 Wamoabu wataangamizwa, wasiwe tena taifa,kwa sababu walijikweza dhidi ya Mwenyezi-Mungu.
43 Kitisho, mashimo na mtego,vinawasubiri enyi watu wa Moabu.Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
44 Atakayetoroka kitishoatatumbukia shimoni;atakayetoka shimoniatanaswa mtegoni.Kwa maana nitaleta mambo hayo juu ya Moabu,katika mwaka wao wa adhabu.Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
45 Wakimbizi wachovu wanatua Heshboni kutaka usalama,maana moto umezuka huko mjini;mwali wa moto toka ikulu ya mfalme Sihoni;umeteketeza mipaka ya Moabu,umeunguza milima yao hao watukutu.
46 Ole wenu watu wa Moabu!Watu wa Kemoshi sasa mmeangamizwa,wana wenu wamechukuliwa mateka,binti zenu wamepelekwa uhamishoni.
47 Lakini siku zijazonitamstawisha tena Moabu.Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.Hii ndiyo hukumu juu ya Moabu.”