1 Mwenyezi-Mungu asema: “Wakati utakuja ambapo nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli nao watakuwa watu wangu.
2 Mimi Mwenyezi-Mungu nasema:Watu walionusurika kuuawaniliwaneemesha jangwani.Wakati Israeli alipotafuta kupumzika,
3 mimi Mwenyezi-Mungu nilimtokea kwa mbali.Nami nimekupenda kwa mapendo ya daima,kwa hiyo nimeendelea kuwa mwaminifu kwako.
4 Nitakujenga upya nawe utajengeka,ewe Israeli uliye mzuri!Utazichukua tena ngoma zakoucheze kwa furaha na shangwe.
5 Utapanda tena mizabibujuu ya milima ya Samaria;wakulima watapanda mbeguna kuyafurahia mazao yake!
6 Maana siku yaja ambapo mlinzi atapiga mbiukatika vilima vya Efraimu:‘Amkeni, twende juu mpaka Siyonikwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’”
7 Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Imbeni kwa furaha kwa ajili ya Yakobo,pigeni vigelegele kwa ajili ya taifa kuu,tangazeni, shangilieni na kusema:‘Mwenyezi-Mungu na awaokoe watu wake,amewaletea ukombozi waliobaki wa Israeli!’
8 Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini,nitawakusanya kutoka miisho ya dunia.Wote watakuwapo hapo;hata vipofu na vilema,wanawake waja wazito na wanaojifungua;umati mkubwa sana utarudi hapa.
9 Watarudi wakiwa wanatoa machozi,nitawarudisha nikiwafariji;nitawapitisha kando ya vijito vya maji,katika njia iliyonyoka ambamo hawatajikwaa;maana mimi nimekuwa baba wa Israeli,Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.
10 Enyi mataifa, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu,litangazeni katika nchi za mbali,semeni: ‘Aliyemtawanya Israeli, atamkusanya,atamtunza kama mchungaji atunzavyo kondoo wake.’
11 Maana mimi Mwenyezi-Mungu nimemkomboa Yakobo,nimemwokoa kutoka kwa wenye nguvu kuliko yeye.
12 Watakuja na kuimba kwa sauti juu ya mlima Siyoni,wataona fahari juu ya wema wangu mimi Mwenyezi-Mungu,kwa nafaka, divai na mafuta niwapavyo,kwa kondoo na ng'ombe kadhalika;maisha yao yatakuwa kama bustani iliyotiliwa maji,wala hawatadhoofika tena.
13 Ndipo wasichana wao watafurahi na kucheza,vijana na wazee watashangilia kwa furaha.Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,nitawafariji na kuwapa furaha badala ya huzuni.
14 Nitawashibisha makuhani kwa vinono,nitawaridhisha watu wangu kwa wema wangu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
15 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Sauti imesikika mjini Rama,maombolezo na kilio cha uchungu.Raheli anawalilia watoto wake,wala hataki kufarijiwa kwa ajili yao,maana wote hawako tena.
16 Sasa, acha kulia,futa machozi yako,kwani utapata tuzo kwa kazi yako,mimi Mwenyezi-Mungu nimesema;watoto wenu watarudi kutoka nchi ya maadui zenu.
17 Yapo matumaini kwa siku zenu zijazo,mimi Mwenyezi-Mungu nimesema;kwani watoto wenu watarejea nchini mwao.
18 “Nimesikia Efraimu akilalamika:‘Umenichapa ukanifunza nidhamu,kwani nilikuwa kama ndama asiyezoea nira.Unigeuze nami nitakugeukia,kwani wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.
19 Maana baada ya kukuasi, nilitubu,na baada ya kufunzwa, nilijilaumu,nikaona haya na kuaibika,maana lawama za ujana wangu ziliniandama.’
20 “Efraimu ni mwanangu mpendwa;yeye ni mtoto wangu nimpendaye sana.Ndio maana kila ninapomtisha,bado naendelea kumkumbuka.Moyo wangu wamwelekea kwa wema;hakika nitamhurumia.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21 “Weka alama katika njia zako,simika vigingi vya kukuongoza,ikumbuke vema ile njia kuu,barabara uliyopita ukienda.Ewe Israeli rudi,rudi nyumbani katika miji yako.
22 Utasitasita mpaka liniewe binti usiye mwaminifu?Maana, mimi nimefanya kitu kipya duniani:Mwanamke amtafuta mwanamume.”
23 Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nitakapowafanikisha tena watu wa Israeli, wao watatangaza tena katika nchi ya Yuda na katika miji yake wakisema:‘Mwenyezi-Mungu akubariki ewe makao adili,akubariki ee mlima mtakatifu!’
24 “Ndipo watu wa Yuda na miji yake yote, wakulima na wachungaji wanaopitapita na makundi yao, watakaa huko pamoja.
25 Waliochoka nitawachangamsha, na walegevu nitawapa nguvu.
26 Ndio maana mtu ataweza kusema: ‘Niliamka nikatambua kwamba usingizi wangu ulinifaa sana.’”
27 Mwenyezi-Mungu asema: “Tazama, siku zaja ambapo nitaijaza nchi ya Israeli na nchi ya Yuda watu na wanyama kama mkulima asiavyo mbegu.
28 Na kadiri nilivyokuwa mwangalifu kuwangoa, kuwabomoa, kuwaangusha, kuwaharibu na kuwatesa, ndivyo nitakavyokuwa mwangalifu kuwapanda na kuwajenga.
29 Siku hizo watu hawatasema tena:‘Wazee walikula zabibu chungu,na meno ya watoto yakatiwa ganzi.’
30 La! Kila mmoja atakufa kwa sababu ya dhambi zake mwenyewe; ni yule tu atakayekula zabibu mbivu ndiye meno yake yatatiwa ganzi.”
31 Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na watu wa Yuda.
32 Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na wazee wao nilipowatoa kwa mkono wangu kutoka Misri; agano hilo walilivunja, ingawa mimi nilikuwa Bwana wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
33 Baada ya siku hizo, nitafanya agano lifuatalo na Waisraeli: Nitaiweka sheria yangu ndani yao, na kuiandika katika mioyo yao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
34 Wala haitawabidi kufundishana na kusema: ‘Mjue Mwenyezi-Mungu’, kwa sababu wote, wadogo kwa wakubwa, watanijua mimi Mungu. Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.”
35 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi, aliyepanga jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku, na aifanyaye bahari iwe na mawimbi:
36 Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi hulifanya jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku; pia mimi huitikisa bahari, nayo hutoa mawimbi. Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Basi, nami nasema: Kadiri ninavyotegemeza mipango hiyo yote yangu kadiri hiyohiyo Israeli watakavyobaki kuwa watu wangu.
37 Kama mbingu zaweza kupimwa, na misingi ya dunia kuchunguzwa, basi, nitawatupilia mbali wazawa wa Israeli, kwa sababu ya mambo yote waliyotenda. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
38 Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo mji huu wa Yerusalemu utajengwa upya kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu, kutoka mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni.
39 Nayo kamba ya kupimia itanyoshwa moja kwa moja hadi mlima Garebu, kisha itazungushwa hadi Goa.
40 Bonde lote walimozikwa wafu na kutupiwa majivu, mashamba yote, mpaka kijito cha Kidroni, mpaka pembe ya lango la Farasi kuelekea mashariki, litakuwa eneo takatifu kwa Mwenyezi-Mungu. Hakuna kitakachoharibiwa humo wala kubomolewa tena milele.”