13 Mbele ya watu wote hao, nilimpa Baruku maagizo yafuatayo:
14 Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Chukua hati hizi zote mbili, hati hii ya kumiliki shamba iliyotiwa sahihi, na hii nyingine iliyo wazi, uziweke katika chungu ili zipate kuhifadhiwa kwa muda mrefu.”
15 Maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nyumba na mashamba, pamoja na mashamba ya mizabibu katika nchi hii yatanunuliwa tena.”
16 Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria, hati ya kumiliki shamba nilimwomba Mwenyezi-Mungu nikisema:
17 Ee Mwenyezi-Mungu, ni wewe ambaye kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu, umeziumba mbingu na dunia; hakuna kisichowezekana kwako.
18 Wewe unaonesha fadhili zako kwa maelfu ya watu; lakini pia unawaadhibu watu kwa sababu ya dhambi za wazee wao. Wewe ni Mungu mkuu, mwenye nguvu, Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lako.
19 Wewe unapanga kwa hekima na unafanya maajabu; njia za watu wote ziko wazi mbele yako, unamlipa kila mmoja kadiri ya njia zake na matendo yake.