10 Viongozi wote na watu wote waliofanya agano hilo walikubaliana wote wawaachie huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na mtu yeyote asiwafanye tena kuwa watumwa. Walikubaliana, wakawaacha huru.
11 Lakini baadaye walibadili nia zao, wakawashika tena watumwa hao wa kiume na wa kike ambao walikuwa wamewaacha huru, wakawafanya watumwa.
12 Hapo neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia:
13 “Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nilifanya agano na wazee wenu nilipowatoa nchini Misri ambako walikuwa watumwa, nikawaambia:
14 ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu atamwacha huru ndugu yake Myahudi aliyeuzwa akawa mtumwa kwa muda wa miaka sita. Mnapaswa kuwaacha huru, wasiwatumikie tena.’ Lakini wazee wenu hawakunisikiliza wala kunitegea sikio.
15 Hivi karibuni nyinyi mlitubu, mkafanya mambo yaliyo sawa mbele yangu, mkawaacha huru Waisraeli wenzenu na kufanya agano mbele yangu katika nyumba yangu.
16 Lakini baadaye mligeuka, mkalitia unajisi jina langu, wakati mlipowachukua tena watumwa walewale wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaachia kama walivyotaka, mkawalazimisha kuwa watumwa tena.