22 Mwenyezi-Mungu asema:“Watu wangu ni wapumbavu,hawanijui mimi.Wao ni watoto wajinga;hawaelewi kitu chochote.Ni mabingwa sana wa kutenda maovu,wala hawajui kutenda mema.”
23 Niliiangalia nchi, lo! Imekuwa mahame na tupu;nilizitazama mbingu, nazo hazikuwa na mwanga.
24 Niliiangalia milima, lo, ilikuwa inatetemeka,na vilima vyote vilikuwa vinayumbayumba.
25 Nilikodoa macho wala sikuona mtu;hata ndege angani walikuwa wametoweka.
26 Niliona nchi yenye rutuba imekuwa jangwa,na miji yake yote imekuwa magofu matupu,kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu.
27 Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Nchi nzima itakuwa jangwa tupu;lakini sitaiharibu kabisa.
28 Kwa hiyo, nchi itaomboleza,na mbingu zitakuwa nyeusi.Maana, nimetamka na sitabadili nia yangu;nimeamua, wala sitarudi nyuma.