20 Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume kwa wanawake, yaani watu wote waliompa jibu hilo:
21 “Kuhusu matambiko ambayo nyinyi na wazee wenu, wafalme wenu na viongozi wenu, pamoja na wananchi wote, mlifanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu, je, mnadhani Mwenyezi-Mungu amesahau au hakumbuki?
22 Mwenyezi-Mungu hakuweza kuvumilia tena matendo yenu maovu na mambo ya kuchukiza mliyotenda; ndiyo maana nchi yenu imekuwa ukiwa, jangwa, laana na bila wakazi, kama ilivyo mpaka leo.
23 Maafa haya yamewapata mpaka leo kwa sababu mliitolea sadaka za kuteketezwa miungu mingine na kumkosea Mwenyezi-Mungu, mkakataa kutii sauti yake au kufuata sheria yake, kanuni zake na maagizo yake.”
24 Yeremia aliwaambia watu wote na wanawake wote: “Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi watu wa Yuda wote mlioko nchini Misri.
25 Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Nyinyi pamoja na wake zenu mmetekeleza kwa vitendo yale mliyotamka kwa vinywa vyenu, mkisema kwamba mmepania kutimiza viapo vyenu mlivyofanya vya kumtolea sadaka na kummiminia kinywaji malkia wa mbinguni. Haya basi! Shikeni viapo vyenu na kutoa sadaka za vinywaji!
26 Lakini sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi watu wote wa Yuda mnaokaa nchini Misri. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Naapa kwa jina langu kuu kwamba hakuna mtu yeyote wa Yuda katika nchi yote ya Misri atakayelitumia jina langu kuapa nalo akisema: ‘Kama aishivyo Bwana Mwenyezi-Mungu!’