25 Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Nyinyi pamoja na wake zenu mmetekeleza kwa vitendo yale mliyotamka kwa vinywa vyenu, mkisema kwamba mmepania kutimiza viapo vyenu mlivyofanya vya kumtolea sadaka na kummiminia kinywaji malkia wa mbinguni. Haya basi! Shikeni viapo vyenu na kutoa sadaka za vinywaji!
26 Lakini sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi watu wote wa Yuda mnaokaa nchini Misri. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Naapa kwa jina langu kuu kwamba hakuna mtu yeyote wa Yuda katika nchi yote ya Misri atakayelitumia jina langu kuapa nalo akisema: ‘Kama aishivyo Bwana Mwenyezi-Mungu!’
27 Mimi nawachungulia hao sio kwa mema bali kwa mabaya. Watu wote wa Yuda nchini Misri wataangamizwa kwa upanga na njaa, asibaki hata mtu mmoja.
28 Ni wachache watakaonusurika vitani na kurudi kutoka nchi ya Misri na kwenda nchini Yuda. Hapo watu wa Yuda wote waliobaki kati ya wale waliokwenda kukaa Misri watatambua ni tamko la nani lenye nguvu: Langu au lao!
29 Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba nitawaadhibu hapahapa mpate kujua kwamba maneno ya maafa niliyotamka dhidi yenu yatatimia. Na hii itakuwa ishara yake:
30 Nitamtia Farao Hofra mfalme wa Misri, mikononi mwa madui zake, mikononi mwa wale wanaotaka kumwua, kama vile nilivyomtia Sedekia mfalme wa Yuda, mikononi mwa adui yake yaani Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, ambaye alitaka kumwua. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”