16 Watu wote nchini watampa sadaka hizo mtawala wa Israeli.
17 Itakuwa ni wajibu wa mtawala kuhakikisha kuwa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zinazotolewa wakati wa sikukuu, mwezi mwandamo, sabato, na sikukuu zozote zilizowekwa zinapatikana kwa Waisraeli. Mtawala mwenyewe ataandaa sadaka za kuondoa dhambi, sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani ili kuwafanyia upatanisho watu wote wa Israeli.
18 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, mtatambika fahali mdogo asiye na dosari ili kutakasa maskani yangu.
19 Kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuipaka miimo ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kona za madhabahu, na miimo ya nafasi ya kuingilia kwenye ua wa ndani.
20 Atafanya vivyo hivyo siku ya saba ya mwezi huo, kwa ajili ya kila mtu aliyetenda dhambi bila kukusudia au kwa kutojua. Kwa njia hiyo mtaitakasa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
21 “Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, mtaadhimisha sikukuu ya Pasaka. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu.
22 Siku hiyo, mtawala atatoa fahali mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote wa Israeli.