1 “Dhambi ya watu wa Yuda, imeandikwa kwa kalamu ya chuma; kwa ncha ya almasi imechorwa mioyoni mwao na katika pembe za madhabahu zao,
2 wakati watu wake wanakumbuka madhabahu zao na sanamu za mungu wa kike, Ashera, zilizowekwa kando ya miti mibichi juu ya vilele vya vilima,
3 na juu ya milima katika sehemu tambarare. Mali yenu na hazina zenu zote nitazitoa zitekwe nyara kulipia dhambi zenu mlizotenda kila mahali nchini mwenu.
4 Itawabidi muiachilie hiyo nchi yenu niliyowapeni, nami nitawafanya muwatumikie maadui zenu katika nchi msiyoijua, kwa sababu hasira yangu imewaka moto usiozimika milele.”
5 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Alaaniwe mtu anayemtegemea binadamu,mtu ambaye anategemea nguvu za binadamu,mtu ambaye moyo wake umeniacha mimi Mwenyezi-Mungu.
6 Huyo ni kama kichaka jangwani,hataona chochote chema kikimjia.Ataishi mahali pakavu nyikani,katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.