1 Ifuatayo ni barua ambayo nabii Yeremia aliwapelekea kutoka Yerusalemu wazee na makuhani, manabii na watu ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kutoka Yerusalemu akawapeleka uhamishoni Babuloni.
2 Yeremia aliiandika barua hiyo baada ya mfalme Yekonia na mama mfalme, matowashi, wakuu wa Yuda na Yerusalemu, mafundi na wahunzi kuondoka Yerusalemu.
3 Barua hii ilipelekwa na Elasa mwana wa Shafani, na Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni. Yeremia aliandika hivi:
4 “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi kuhusu mateka wote aliowaacha wachukuliwe kutoka Yerusalemu hadi Babuloni:
5 ‘Jengeni nyumba mkae. Limeni mashamba, pandeni mbegu na kula mazao yake.
6 Oeni wake, mpate watoto; waozeni wana wenu na binti zenu nao pia wapate watoto. Ongezekeni na wala msipungue.