18 Nitawaandama kwa upanga, njaa na maradhi mabaya. Nitawafanya kuwa kitu cha kuchukiza kwa tawala zote za dunia, naam, kitu cha laana, kioja, dharau na kitu cha kupuuzwa katika mataifa yote nilikowafukuzia.
19 Nitafanya hivyo kwa sababu hamkusikiliza maneno yangu niliyowaambia kila mara kwa njia ya watumishi wangu, manabii, nanyi mkakataa kusikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
20 Enyi nyote niliowatoa kutoka Yerusalemu, nikawapeleka uhamishoni Babuloni, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu.”
21 Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi juu ya Ahabu mwana wa Kolaya, na juu ya Sedekia mwana wa Maaseya, ambao wanawatabirieni uongo kwa jina lake: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, naye atawaua mkiona kwa macho yenu wenyewe.
22 Kwa sababu jambo hilo litakalowapata, watu wote waliohamishiwa Babuloni kutoka Yerusalemu watatumia msemo huu wa kulaania: Mwenyezi-Mungu akufanye kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babuloni aliwachoma motoni.
23 Kisa ni kwamba walitenda mambo ya aibu katika Israeli. Walizini na wake za jirani zao, na kusema maneno ya uongo kwa jina langu, jambo ambalo mimi sikuwaamuru walifanye. Mimi nayajua hayo; nimeyashuhudia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
24 Mwenyezi-Mungu aliniagiza nimwambie hivi Shemaya wa Nehelamu: