11 Lakini Nebukadneza, mfalme wa Babuloni alipofika, kuishambulia nchi hii, tuliamua kuja Yerusalemu ili tuliepe jeshi la Wakaldayo na la Waashuru. Kwa hiyo sasa tunaishi mjini Yerusalemu.”
12 Kisha neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia:
13 “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu hivi: Je, nyinyi hamwezi kupokea mafundisho na kusikia maneno yangu?
14 Ile amri ambayo Yonadabu mwana wa Rekabu, aliwapa wanawe, kwamba wasinywe divai, imefuatwa; nao hawanywi divai mpaka siku hii ya leo, maana wametii amri ya mzee wao. Lakini mimi niliongea nanyi tena na tena, nanyi hamkunisikiliza.
15 Niliwapelekea tena na tena watumishi wangu wote yaani manabii wawaambieni kila mmoja wenu aachane na mwenendo wake mwovu, arekebishe matendo yake na kuacha kuifuata na kuitumikia miungu mingine. Na kwamba mkifanya hivyo mtakaa katika nchi niliyowapa nyinyi na wazee wenu. Lakini nyinyi hamkunitegea sikio wala hamkunisikiliza.
16 Wana wa Yonadabu mwana wa Rekabu, wameshika amri waliyopewa na mzee wao; lakini nyinyi hamkunitii.
17 Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Ninawaletea watu wa Yuda na wakazi wote wa Yerusalemu maovu yote niliyotamka dhidi yao, kwa sababu mimi niliongea nao, lakini hawakunisikiliza; niliwaita, lakini hawakuniitikia.”