3 Mwenyezi-Mungu asema kuwa hakika mji huu utatiwa mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babuloni na kutekwa.”
4 Wakuu wakamwambia mfalme, “Yafaa mtu huyu auawe kwa maana anawavunja moyo askari ambao wameachwa katika mji huu na watu wote kwa jumla, kwa kusema maneno kama hayo. Yeye hawatakii watu hawa mema bali mabaya.”
5 Mfalme Sedekia akasema, “Haya! Mtu huyu yumo mikononi mwenu; mimi siwezi kuwapinga.”
6 Basi, wakamchukua Yeremia wakamtumbukiza katika kisima cha Malkia mwana wa mfalme ambacho kilikuwa katika ukumbi wa walinzi. Walimshusha Yeremia ndani kwa kamba. Ndani ya kisima hicho hakukuwa na maji bali tope, naye Yeremia akazama katika tope.
7 Lakini Ebedmeleki, towashi Mwethiopia aliyekuwa akifanya kazi katika ikulu, alipata habari kwamba walikuwa wamemtumbukiza Yeremia kisimani. Wakati huo mfalme alikuwa anabarizi penye lango la Benyamini.
8 Basi, Ebedmeleki akamwendea mfalme, akamwambia,
9 “Bwana wangu mfalme, watu hawa wamefanya kitu kibaya. Wamemtumbukiza yule nabii Yeremia kisimani ambamo kwa kweli atakufa kwa njaa, kwa maana hamna chakula tena mjini.”