9 Kisha, Nebuzaradani, kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni Babuloni watu waliokuwa wamebaki mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwake pamoja na watu wote waliokuwa wamebaki.
10 Nebuzaradani, kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwaacha katika nchi ya Yuda baadhi ya watu maskini ambao hawakuwa na chochote, akawagawia mashamba ya mizabibu na kuwapa maeneo ya kulima wakati huohuo.
11 Nebukadneza mfalme wa Babuloni alikuwa amempa Nebuzaradani kapteni wa walinzi, amri ifuatayo kuhusu Yeremia:
12 “Mchukue Yeremia, umtunze vema wala usimdhuru; mtendee kama anavyokuambia.”
13 Basi, Nebuzaradani kapteni wa walinzi, Nebushani, Nergal-shareza pamoja na maofisa wakuu wote wa mfalme wa Babuloni, wakatuma watu wamtoe Yeremia ukumbini mwa walinzi.
14 Wakamkabidhi Yeremia kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, amchukue nyumbani kwake. Basi, Yeremia akaishi pamoja na wananchi wengine.
15 Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia wakati alipokuwa amefungwa katika ukumbi wa walinzi: