10 Mpaka hivi leo hamjajinyenyekesha wala kuogopa wala kuzifuata sheria zangu na kanuni zangu nilizowawekea nyinyi na wazee wenu.
11 “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Haya! Nitawageukia niwaleteeni maafa na kuiangamiza Yuda yote.
12 Nitawaondoa watu wa Yuda waliosalia ambao wamepania kwenda kukaa Misri, na kuwaangamiza wote, wakubwa kwa wadogo; watakufa kwa upanga au kwa njaa. Watakuwa takataka, kitisho, laana na dhihaka.
13 Nitawaadhibu wale wanaokaa katika nchi ya Misri kama nilivyouadhibu mji wa Yerusalemu, kwa vita, njaa, na maradhi mabaya.
14 Kwa hiyo hapatakuwa na mtu hata mmoja kati ya watu wa Yuda waliosalia na kwenda kukaa katika nchi ya Misri ambaye atanusurika au kuishi au kurudi katika nchi ya Yuda ambayo wanatamani kurudi na kuishi humo. Hawatarudi, isipokuwa baadhi ya wakimbizi.”
15 Kisha, wanaume wote waliojua kwamba wake zao walikuwa wameifukizia ubani miungu mingine, na wanawake wote waliokuwa hapo, kusanyiko kubwa la watu, pamoja na Waisraeli waliokuwa wanakaa Pathrosi katika nchi ya Misri walimjibu Yeremia:
16 “Jambo hilo ulilotuambia kwa niaba ya Mwenyezi-Mungu hatutalitii.