9 Basi Wakaldayo walimteka mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni, huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu.
10 Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda.
11 Kisha aliyangoa macho ya Sedekia na kumfunga pingu, akamchukua Sedekia Babuloni na kumtia kizuizini mpaka siku alipokufa.
12 Katika siku ya kumi ya mwezi wa tano, mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme ambaye alimtumikia mfalme wa Babuloni, aliingia Yerusalemu.
13 Alichoma moto nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu na nyumba zote za Yerusalemu; kila nyumba kubwa ilichomwa moto.
14 Askari wote wa Wakaldayo waliokuwa pamoja na kapteni wa walinzi, walizibomoa kuta zote zilizouzunguka mji wa Yerusalemu.
15 Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na mafundi.