20 Enyi watu wa Yerusalemu,pandeni Lebanoni mpige kelele,pazeni sauti zenu huko Bashani;lieni kutoka milima ya Abarimu,maana wapenzi wenu wote wameangamizwa.
21 Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi mlipokuwa na fanaka,lakini nyinyi mkasema, “Hatutasikiliza.”Hii ndiyo tabia yenu tangu ujana wenu,hamjapata kuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu.
22 Viongozi wenu watapeperushwa na upepo,wapenzi wenu watachukuliwa uhamishoni.Ndipo mtakapoona haya na kufadhaika,kwa sababu ya uovu wenu wote mliotenda.
23 Enyi wakazi wote wa Lebanoni,nyinyi mkaao salama kati ya mierezi;jinsi gani mtakavyopiga kite uchungu utakapowakumba,uchungu kama wa mama anayejifungua!
24 Na kuhusu Konia mfalme wa Yuda, mwanawe Yehoyakimu, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Naapa kwa nafsi yangu mimi Mwenyezi-Mungu kwamba hata kama wewe Konia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya mhuri katika mkono wangu wa kulia, ningekuvulia mbali.
25 Nitakutia mikononi mwa wale wanaotaka kuyamaliza maisha yako; naam, mikononi mwa wale unaowaogopa, mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni; naam, mikononi mwa Wakaldayo.
26 Nitakufukuzia mbali katika nchi ya kigeni, wewe pamoja na mama yako mzazi. Mtakuwa watumwa katika nchi hiyo ambamo nyote wawili hamkuzaliwa, nanyi mtafia hukohuko.