2 “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Nimeivunja nira ya mfalme wa Babuloni.
3 Mnamo miaka miwili nitavirudisha hapa vyombo vyote vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Nebukadneza, mfalme wa Babuloni alivichukua na kuvipeleka Babuloni.
4 Pia nitamrudisha Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na watu wote wa Yuda waliohamishiwa Babuloni. Naam, nitaivunja nira ya mfalme wa Babuloni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
5 Kisha, nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania mbele ya makuhani na watu wote waliokuwa wamesimama katika hekalu la Mwenyezi-Mungu:
6 “Na iwe hivyo! Mwenyezi-Mungu na afanye hivyo. Mwenyezi-Mungu na ayatimize maneno uliyotabiri, avirudishe hapa vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kutoka Babuloni pamoja na watu wote waliohamishiwa huko.
7 Lakini sikiliza neno ninalokuambia wewe na watu wote.
8 Manabii waliotutangulia mimi na wewe, tangu zamani za kale, walitabiri kwamba vita, njaa na maradhi vitazikumba nchi nyingi na tawala kubwa.