34 Waliweka sanamu za miungu yao ya kuchukiza katika nyumba hii inayojulikana kwa jina langu, wakaitia unajisi.
35 Walimjengea mungu Baali madhabahu katika bonde la Mwana wa Hinomu, ili wamtolee mungu Moleki wavulana wao na binti zao, ingawa sikuwaamuru wala sikufikiria kwamba wangefanya hivyo, wakawafanya watu wa Yuda watende dhambi.”
36 Sasa basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Yeremia, watu hawa wanasema kwamba, kwa vita, njaa na maradhi, mji huu utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babuloni. Lakini nasema:
37 Nitawakusanya watu kutoka nchi zote ambako kwa hasira na ghadhabu na chuki yangu kubwa, niliwatawanya. Nitawarudisha tena mahali hapa, na kuwafanya wakae salama.
38 Nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
39 Nitawapa moyo mmoja na nia moja, wapate kunicha mimi daima, kwa faida yao wenyewe na kwa faida ya watoto wao watakaofuata.
40 Nitafanya nao agano la milele, kwamba sitaacha kamwe kuwatendea mema; nitaweka mioyoni mwao uchaji wangu ili wasiniache tena.