2 Na katika siku ya tisa ya mwezi wa nne, mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa.
3 (Basi maofisa wakuu wafuatao wa mfalme wa Babuloni waliingia na kukaa kwenye lango la katikati: Nergal-shareza, Samgar-nebo, Sar-sekimu mkuu wa matowashi na Nergal-shareza mkuu wa wanajimu, pamoja na maofisa wengine wote wa mfalme wa Babuloni.)
4 Naye Sedekia, mfalme wa Yuda na askari wake wote walipowaona, walitoroka. Walitoka nje ya mji usiku, wakipitia katika bustani ya mfalme, kwenye lango katikati ya kuta mbili, wakaenda upande wa Araba.
5 Lakini jeshi la Wakaldayo liliwafuatia na kumteka Sedekia katika tambarare za Yeriko. Baada ya kumchukua walimfikisha kwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu.
6 Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda.
7 Kisha alingoa macho yake Sedekia na kumfunga pingu, ili ampeleke Babuloni.
8 Wakaldayo waliichoma moto ikulu na nyumba za watu; pia walizibomoa kuta za Yerusalemu.