1 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Ukitaka kurudi ee Israeli, nirudie mimi.Ukiviondoa vitu vya kuchukiza mbele yangu,usipotangatanga huko na huko,
2 ukiapa kwa ukweli, unyofu na uadilifu,kwa kusema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo’,ndipo mataifa yatakapopata baraka kwangu,na kutukuka kwa sababu yangu.”
3 Mwenyezi-Mungu awaambia hivi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu:“Limeni mashamba yenu mapya;msipande mbegu zenu penye miiba.
4 Enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu,jitakaseni kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu,wekeni mioyo yenu wazi mbele yangu.La sivyo, ghadhabu yangu itachomoza kama moto,iwake hata pasiwe na mtu wa kuizima,kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.
5 “Tangazeni huko Yuda,pazeni sauti huko Yerusalemu!Pigeni tarumbeta kila mahali nchini!Pazeni sauti na kusema:Kusanyikeni pamoja!Kimbilieni miji yenye ngome!