10 Kama mtabaki katika nchi hii, basi, nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawaotesha wala sitawangoa; kwa maana nitabadili nia kwa sababu ya maafa niliyowatenda.
11 Msimwogope mfalme wa Babuloni mnayemwogopa; naam, msimwogope hata kidogo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi niko pamoja nanyi kuwaokoeni na kuwasalimisha kutoka mikononi mwake.
12 Nitawahurumieni na kumfanya mfalme awahurumie na kuwaacha nchini mwenu.
13 “Lakini mkisema: ‘Hatutaki kubaki katika nchi hii,’ na hivyo mkaacha kutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
14 na kusema kwamba mtakwenda kukaa nchini Misri, ambako hamtaona vita wala kusikia sauti ya tarumbeta wala kukosa chakula,
15 basi, sikilizeni asemavyo Mwenyezi-Mungu enyi mabaki ya Yuda. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama mmekusudia kuingia nchini Misri na kukaa huko,
16 basi, vita mnavyoviogopa vitawakumba hukohuko Misri, na njaa mnayoihofia itawaandama vikali hadi Misri, na mtafia hukohuko.