5 Kisha, watu wakamwambia Yeremia, “Mwenyezi-Mungu na awe shahidi wa kweli na mwaminifu dhidi yetu ikiwa hatutafanya jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atakavyokuagiza utuambie.
6 Iwe ni jambo la kupendeza au la, sisi tutaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu ambaye tunakutuma kwake ili tufanikiwe tutakapomtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.”
7 Baada ya siku kumi, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia.
8 Basi, Yeremia akamwita Yohanani mwana wa Karea, na makamanda wote wa majeshi pamoja na watu wote, wadogo kwa wakubwa, akawaambia,
9 “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli ambaye mlinituma kwake nipeleke maombi yenu, asema hivi:
10 Kama mtabaki katika nchi hii, basi, nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawaotesha wala sitawangoa; kwa maana nitabadili nia kwa sababu ya maafa niliyowatenda.
11 Msimwogope mfalme wa Babuloni mnayemwogopa; naam, msimwogope hata kidogo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi niko pamoja nanyi kuwaokoeni na kuwasalimisha kutoka mikononi mwake.