8 Sisi tumeitii daima amri hiyo ya mzee wetu Yonadabu mwana wa Rekabu, kuhusu jambo alilotuamuru. Sisi hatunywi kamwe divai; sisi wenyewe hatunywi, wala wake zetu, wala watoto wetu wa kiume au wa kike.
9 Sisi hatujijengei nyumba za kuishi. Hatuna mashamba ya mizabibu wala mashamba ya kulima na kupanda mbegu.
10 Sisi tumeishi katika mahema na kutii mambo yote ambayo Yonadabu, mzee wetu, alituamuru.
11 Lakini Nebukadneza, mfalme wa Babuloni alipofika, kuishambulia nchi hii, tuliamua kuja Yerusalemu ili tuliepe jeshi la Wakaldayo na la Waashuru. Kwa hiyo sasa tunaishi mjini Yerusalemu.”
12 Kisha neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia:
13 “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu hivi: Je, nyinyi hamwezi kupokea mafundisho na kusikia maneno yangu?
14 Ile amri ambayo Yonadabu mwana wa Rekabu, aliwapa wanawe, kwamba wasinywe divai, imefuatwa; nao hawanywi divai mpaka siku hii ya leo, maana wametii amri ya mzee wao. Lakini mimi niliongea nanyi tena na tena, nanyi hamkunisikiliza.