1 Neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kwa njia ya nabii Yeremia kuhusu nchi ya Babuloni na nchi ya Wakaldayo:
2 “Tangazeni kati ya mataifa,twekeni bendera na kutangaza,Msifiche lolote. Semeni:‘Babuloni umetekwa,Beli ameaibishwa.Merodaki amefadhaishwa;sanamu zake zimeaibishwa,vinyago vyake vimefadhaishwa.’
3 “Kwa maana, taifa kutoka kaskazini limefika kuushambulia; litaifanya nchi yake kuwa uharibifu. Hakuna atakeyeishi humo; watu na wanyama watakimbia mbali.
4 “Siku hizo na wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, watu wa Israeli na watu wa Yuda watakusanyika pamoja na kurudi wakilia huku wananitafuta mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
5 Watauliza njia ya kwenda Siyoni, huku nyuso zao zimeelekea huko, wakisema, ‘Njoni!’ Nao watajiunga na Mwenyezi-Mungu katika agano la milele ambalo kamwe halitasahauliwa.
6 “Watu wangu walikuwa kondoo waliopotea; wachungaji wao wamewapotosha, wakawageuza kuelekea milimani; walitembea toka mlima hadi kilima, wakasahau zizi lao.
7 Watu wote waliowakuta waliwaua, na maadui zao wamesema, ‘Hatuna hatia sisi’, maana hao wamemkosea Mwenyezi-Mungu aliye malisho yao ya kweli; Mwenyezi-Mungu ambaye ni tegemeo la wazee wao!