2 Inua macho uvitazame vilele vya vilima!Pako wapi mahali ambapo hawajalala nawe?Uliwangoja wapenzi wako kando ya njia,kama bedui aviziavyo watu jangwani.Umeifanya nchi kuwa najisi,kwa ukahaba wako mbaya kupindukia.
3 Ndiyo maana manyunyu yamezuiliwa,na wala mvua za vuli hazijanyesha.Hata hivyo uko macho makavu kama kahaba,huna haya hata kidogo.
4 “Hivi punde tu si ulinililia ukisema:‘Wewe u baba yangu,ulinipenda tangu utoto wangu?
5 Je, utanikasirikia daima?Utachukizwa nami milele?’Israeli, hivyo ndivyo unavyosema;na kumbe umetenda uovu wote ulioweza.”
6 Wakati wa utawala wa mfalme Yosia, Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Je, umeona jinsi Israeli asiye mwaminifu alivyofanya? Aliniacha, akapanda juu ya kila kilima kirefu na kwenda chini ya kila mti wenye majani mabichi, akafanya ukahaba wake humo!
7 Mimi nilidhani kuwa baada ya kufanya yote hayo, atanirudia. Lakini wapi; hakunirudia. Yuda, dada yake mdanganyifu, alishuhudia yote hayo.
8 Zaidi ya hayo, Yuda alishuhudia kuwa nilimpa Israeli talaka kwa sababu ya ukahaba wake na kwa kukosa uaminifu kwangu. Lakini hata hivyo, Yuda, dada yake mdanganyifu, hakuogopa; naye pia alikwenda na kufanya ukahaba!