21 Lakini kama ukikataa kujitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwao, haya ndiyo maono ambayo Mwenyezi-Mungu amenionesha.
22 Katika maono hayo, niliona wanawake waliobaki katika ikulu ya mfalme wa Yuda wakipelekwa kwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, nao walikuwa wakisema hivi:‘Marafiki zako uliowaamini wamekudanganya,nao wamekushinda;kwa kuwa miguu yako imezama matopeni,wamekugeuka na kukuacha.’
23 Wake zako wote na watoto wako watapelekwa kwa Wakaldayo, nawe mwenyewe hutanusurika. Utachukuliwa mateka na mfalme wa Babuloni na mji huu utateketezwa kwa moto.”
24 Sedekia akamwambia Yeremia: “Mtu yeyote asijue habari hizi, nawe hutauawa.
25 Kama viongozi wakisikia kuwa nimeongea nawe, kisha wakaja na kukuambia, ‘Hebu tuambie, ulizungumza nini na mfalme. Usitufiche chochote nasi hatutakuua’;
26 wewe utawaambia hivi: ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme kwa unyenyekevu asinirudishe gerezani nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafia huko.’”
27 Kisha, viongozi walimjia Yeremia wakamwuliza mambo hayo, naye akawajibu kama mfalme alivyomwelekeza. Ndipo walipoacha kuzungumza naye kwa sababu hakuna mtu aliyekuwa amesikia mazungumzo yake na mfalme.