Yobu 13 BHN

Jibu la Yobu laendelea

1 “Tazama, hayo yote nimeyaona kwa macho yangu;nimeyasikia kwa masikio yangu mwenyewe na kuelewa.

2 Yote mnayoyajua, mimi pia nayajua.Mimi si mtu duni kuliko nyinyi.

3 Lakini ningependa kusema na Mungu mwenye nguvu,natamani kujitetea mbele zake Mungu.

4 Lakini nyinyi mnaupakaa uongo chokaa;nyinyi nyote ni waganga wasiofaa kitu.

5 Laiti mngekaa kimya kabisa,ikafikiriwa kwamba mna hekima!

6 Sikilizeni basi hoja yangu,nisikilizeni ninapojitetea.

7 Je, mnadhani mwamtumikia Mungu kwa kusema uongo?Mnafikiri kusema kwa hila kunamfaa yeye?

8 Je, mnajaribu kumpendelea Mungu?Je, mtamtetea Mungu mahakamani?

9 Je, akiwakagua nyinyi mtapona?Au mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu kama watu?

10 Hakika yeye atawakemeakama mkionesha upendeleo kwa siri.

11 Je, fahari yake haiwatishi?Je, hampatwi na hofu juu yake?

12 Misemo yenu ni methali za majivu,hoja zenu ni ngome za udongo.

13 “Nyamazeni, nami niongee.Yanipate yatakayonipata.

14 Niko tayari hata kuhatarishamaisha yangu;

15 Mungu aniue akitaka, sina la kupoteza,hata hivyo nitautetea mwenendo wangu mbele yake.

16 Kama nikifaulu hapo nitakuwa nimeshinda,maana mtu mwovu hawezi kwenda mbele yake.

17 Sikilizeni kwa makini maneno yangu,maelezo yangu na yatue masikioni mwenu.

18 Kesi yangu nimeiandaa vilivyo,nina hakika mimi sina hatia.

19 “Nani atakayeipinga hoja yangu?Niko tayari kunyamaza na kufa.

20 Mungu wangu, nijalie tu haya mawili,nami sitajificha mbali na wewe:

21 Kwanza uniondolee mkono wako unaonipiga,na usiniangamize kwa kitisho chako.

22 “Uanze kutoa hoja yako nami nikujibu.Au mimi nianze, nawe unijibu.

23 Makosa na dhambi zangu ni ngapi?Nijulishe hatia na dhambi yangu.

24 “Mbona unaugeuza uso wako mbali nami?Kwa nini unanitendea kama adui yako?

25 Je, utalitisha jani linalopeperushwa,au kuyakimbiza makapi?

26 Wewe umetoa mashtaka makali dhidi yangu,na kunibebesha dhambi za ujana wangu.

27 Wanifunga minyororo miguuni,wazichungulia hatua zangu zote,na nyayo zangu umeziwekea kikomo.

28 Nami naishia kama mti uliooza,mithili ya vazi lililoliwa na nondo.